Wanawake Urusi watakiwa kutofanya mapenzi na raia wa kigeni
Mbunge mmoja nchini Urusi anasema kuwa wanawake hawafai kufanya mapenzi na wageni wakati wa kombe la dunia huku akionya kuhusu watoto wanaozaliwa kutoka rangi tofauti. Tamara Plentyova mkuu wa kamati ya familia, wanawake na masuala ya watoto bungeni, alisema kuwa hata iwapo uhusiano huo utasababisha kufanyika kwa harusi, wanawake au watoto wao watachukuliwa na nwanamume huyo ambaye atakuwa raia wa kigeni. Mbunge huyo ni wa chama cha Kikomunisti, ''Hata wakiolewa, watawachukua, halafu watashindwa namna ya kurudi," Bi Pletnyova alisema katika kituo cha Govorit Moskva. "Baadaye watakuja kwangu, wasichana wakilia kwamba watoto wao wamechukuliwa''. Alisema kuwa wanawake waliopata watoto na raia wa kigeni wakati wa michezo ya Olimpiki ya 1980 mjini Moscow walisalia kuwa wanawake wasio na wanaume. ''Ni vyema iwapo ni mtu wa rangi inayofanana na yako lakini iwapo ni mtu wa rangi tofauti basi kunakuwa na shida''. ''