Ukeketaji Manyara yaongoza

Hali ya Ukeketaji mkoa wa Manyara imefikia asilimia 70.8 kutoka asilimia 58 mwaka jana,hali ambayo ni mbaya zaidi licha ya jitihada za serikali na Mashirika binafsi kutoa elimu juu ya madhara ya kufanya ukeketaji.
Hali ya Ukeketaji katika mkoa wa Manyara bado ni tatizo kutokana na watoto wachanga pia kufanyiwa vitendo vya ukeketaji kwa siri pale wanapozaliwa.

Anna Emmanuel Fisoo afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Manyara anaeleza kuwa tatizo la ukeketaji kwa wanawake na watoto bado lipo katika maeneo mengi ya mkoa katika baadhi ya makabila ya wafugaji.

Amesema ukatili mwingine wanaofanyiwa watoto ni ulawiti na kubakwa na kwamba kesi nyingi zipo Mahakamani.

Amesema ili kutokomeza ukatili huo ni lazima jamii,taasisi za serikali na mashirika binafsi kila mmoja atimize wajibu wake kwa wakati na kwa kufanya hivyo hali hiyo itakuwa imepungua kwa asiliamia 50 ifikapo mwaka 2022.

Paskalia Changala Mratibu wa shirika linalojishughulisha na masuala ya kutokomeza ukeketaji kwa watoto wa kike na ukatili wa kijinsia [AFNET] anasema hali ya Ukeketaji mkoa wa Manyara kwa takwimu ipo juu kwa asilimia 70.8% na kwa sasa watu  wamegundua mbinu mpya ya kufanya ukeketaji kwa kuwakeketa watoto wachanga.

Aliendelea kusema kwa kusema “zamani walikuwa wakikeketa wakiwa wakubwa lakini kwa sasa wamebadilisha njia”alisema Changala.

Aidha Changala anasema wao kama AFNET wamekuwa wakishirikiana na Serikali kupitia ofisi ya jinsia na Maendeleo ya jamii pamoja na Dawati la jinsia Polisi kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara na mashuleni pamoja na kuwakusanya Mangariba ambao kwa sasa ndio wakunga wa jadi.

Shirika hilo limewataka wanaofanya  kazi hiyo waachane nayo mara moja,watafute mawazo mbadala ya kuwaingizia kipato na sio kutumia viungo vya binadamu.

Wasichana wengi wamekuwa wakipoteza maisha baada ya kufanyiwa Ukeketaji kwa sababu ya kuvuja damu nyingi hivyo basi Muungwana Blog inaiomba jamii zinazofanya vitendo hivyo ziache  na kutii wito wa serikali wa kuacha kukeketa.

Mangariba hao wamekuwa wakipatiwa vitu kama vile mbuzi,ng’ombe na Kondoo na vitu vingine  kama ujira baada ya kufanya kitendo hicho cha ukeketaji kwa wasichana.

Kumbuka Ukeketaji unamnyima haki na uhuru Msichana.

Comments

Popular posts from this blog