Polisi: Tutamkamata na Kumhoji Askofu Kakobe kwa Uchochezi
Licha ya kutokiri moja kwa moja juu ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu kumkamata Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGFC) lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limesema ni lazima litamhoji kiongozi huyo wa kiroho. Kuhojiwa huko kumetokana na kauli yake dhidi ya serikali aliyoitoa wakati wa ibada ya Krismasi. Jana, kulienea taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kueleza kwamba askofu huyo alitiwa mbaroni jana asubuhi na askari wa Jeshi la Polisi huku sababu za kukamatwa zikielezwa kuwa ni ujumbe alioutoa wakati wa mahubiri yake ya ibada ya Krismasi. Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na ukweli wa taarifa za kutiwa mbaroni kwa Askofu Kakobe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa ni kweli walishakuwa katika harakati za kumkamata. “Ametoa maneno ya kashfa katika mahubiri yake, lakini sina taarifa kama amekamatwa,” Kamanda Mambosasa alisema na kuongeza: ...