SHEHA ALIYEKUTWA NA BANGI ATIMULIWA KAZINI HUKO UNGUJA
SERIKALI katika mkoa wa Kusini Unguja, imemtimua kazi Sheha wa Kitumba, Mtwana Kificho, ambaye wiki iliyopita nyumbani kwake alikutwa na majani makavu yanayosadikiwa kuwa bangi baada ya polisi kufanya ukaguzi. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Dk Idrissa Muslim Hijja, jana aliwateuwa masheha wawili na kuwaapisha kuongoza shehia hizo, pamoja na sheha mpya wa Kitumba, Makame Chum. Akizungumza na masheha hao katika eneo la Tunguu katika mkoa wa Kusini Unguja, Dk Hijaa, aliwataka masheha hao kutekeleza majukumu yao ya kuongoza kwa busara katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria. Alisema masheha ni watendaji na wasimamizi wa majukumu ya wananchi, ambapo matatizo yao wanatakiwa kuwasilishwa mbele ya Serikali Kuu kupatiwa ufumbuzi. “Majukumu ya kazi kwa masheha ni kusimamia matatizo ya wananchi na kuyaelekeza kwa Serikali Kuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi na sio kuchochea mifarakano katika jamii,” alisema. ...