Kafulila kuelezea sakata la Tegeta Escrow

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema ataanza kuelezea kwa kina sakata lililotikisa nchi la kashfa ya Tegeta Escrow wiki ijayo kupitia gazeti la Uwazi.

Akizungmza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Kafulila alisema amegundua kuwa kuna mambo mengi ambayo wananchi wanataka kuyajua kuhusu sakata hilo, hivyo ameamua kuyaandika yote ili kiu ya Watanzania kujua kuhusu sakata hilo iishe.

“Najua kwamba mimi ndiye niliyelibebea bango bungeni sakata lile na kwa kuwa Gazeti la Uwazi linasomwa na watu wengi, nimeamua kuyaeleza yote kupitia gazeti hili kuanzia toleo lijalo,” alisema Kafulila.

Alifafanua kuwa wazo la kuandika sakata hilo amelipata baada ya kuulizwa sana na baadhi ya wananchi kwamba liliishaje na jinsi lilivyomfanya akorofishane na vigogo wengi na hata kujihatarishia maisha.

“Kwa kuwa hilo ni jambo zito, ni vema wananchi wajiandae kusoma kwa urefu juu ya sakata hilo kwenye gazeti hili. Nadhani nimefanya uamuzi sahihi,” alisema Kafulila.

Kashfa hiyo ya Tegeta Escrow inahusisha uchotaji wa Sh. 306 bilioni za akaunti ya Escrow, ikahofiwa kuwakumba vigogo zaidi ya 50 ndani ya Serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, majaji na wakuu wa taasisi za Serikali waliohusika.

Enzi hizo aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kuitisha kikao cha mawaziri ambacho kilihudhuriwa na baadhi ya mawaziri na walifikia uamuzi kuwa suala hilo litajadiliwa ndani ya chama kabla ya kuingia ndani ya Bunge.

Aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya Miundombinu, alisema viongozi kama wabunge na mawaziri walitajwa kupiga dili katika akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa (enzi hizo) baadhi ya viongozi wa Serikali walikuwa hawaonyeshi dhamira njema katika kuheshimu misingi ya utawala bora.

Sakata la utoroshwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ambalo liliwaandama baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali lilijitokeza kwa sehemu kubwa katika baadhi ya magazeti ya nchi za Magharibi yaliyohoji jinsi Serikali inavyoingiwa na kigugumizi cha kulipatia ufumbuzi sakata hilo.

Magazeti hayo likiwamo DailyMail la Uingereza lililowahi kufichua kuwapo kwa vitendo vya ufisadi katika uwindaji wa wanyamapori kulikolisababishia taifa hasara kubwa, lilisema kuwa Tanzania inaendelea kuandamwa na jinamizi la ufujaji wa mali ya umma.

DailyMail lilisema wakati huo kuwa, wabunge waliibana Serikali wakitaka kujadiliwa kwa ripoti ya Escrow ili kuliokoa taifa ambalo tayari lilianza kuonja machungu ya kusitishiwa misaada kutoka kwa wafadhili wa kigeni.

Katika ripoti yake hiyo ambayo ililinukuu Shirika la Habari la Reuters, DailyMail lilisema rushwa ni ugonjwa unaoendelea kuiandama Tanzania na kwamba vitendo hivyo sasa vimevuka mipaka na kuwakwaza wawekezaji wa kigeni.

Hata hivyo, uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli imevalia njuga suala la rushwa na wizi wa rasilimali za taifa na kufanya mataifa mengi kummwagia sifa rais kwa kuonekana kuwa anapambana na mianya ya rushwa kwa dhati.

Tayari amedhibiti wizi uliokuwa ukifanyika bandarini na kwenye machimbo ya madini, huku Rais Magufuli akisisitiza kuwa fedha za umma lazima ziogopwe kama sumu.

Comments

Popular posts from this blog