MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula amesema vigezo 13, vitatumika kuwachuja wanachama wa chama hicho ambao wameomba kugombea urais CCM. Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma. Aliwakumbusha watangaza nia kuwa hawaruhusiwi kutoa rushwa, kushawishi au kushawishika kuwapa rushwa wale wanaowadhamini. Vigezo vyenyewe Alitaja vigezo 13 vitakavyotumika kuwachuja wagombea kuwa ni uwezo mkubwa na uzoefu katika uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara. Pia, kuwa na elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na amani. “Anatakiwa kuwa na upeo mkubwa usiotiliwa mashaka kuhusu masuala ya kimataifa, asiye na hulka ya kidikteta au mfashisti, awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala bora,” alisema Mangula. Alitaja vigezo vingine ni kuwa mtetezi wa wanyonge na haki za bin...