RAIS Dk. John Magufuli anaelekea kufunga mwaka huku akiwa amesafisha Serikali yake ya awamu ya tano kwa kuwatumbua watendaji zaidi ya 300 tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana. Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika uozo ndani ya Serikali, huku baadhi ya watendaji wa ngazi za juu wakihusishwa na tuhuma mbalimbali, ikiwamo za matumizi mabaya ya ofisi na ufisadi. Hatua hiyo inaelezwa ni miongoni mwa mkakati wa kuzika mfumo wa Serikali ya awamu ya nne ambao baadhi ya vigogo walikuwa wakifanya mambo holela na kusahau wajibu wao kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Uchukuaji huo wa nidhamu kwa idadi kubwa ya watumishi wa Serikali, inaonyesha kuwa kila siku kuna wastani wa kigogo mmoja mtendaji wa juu ambaye amejikuta akifutwa kazi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutumia madaraka vibaya na kuisababishia hasara Serikali. Fagio hilo linajumuisha watumishi wa Serikali waliosimamishwa kazi kutoka taasisi mbalimbali na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa. Asilimia kub...