Ummy Mwalimu: Marufuku Kuozesha Waliomaliza La 7
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. SERIKALI imewaonya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutowaozesha watoto wote wa kike waliohitimu darasa la saba mwaka huu wakati wa kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao, iwe ni kwa sababu yoyote ile au kwa lengo la kujipatia mali kwa njia ya mahari. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mkono wa serikali kisheria ni mrefu, hivyo wazazi au walezi watakaokwenda kinyume watahakikisha kuwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Ummy ameyasema hayo jana katika tamko maalumu alilolitoa kwa wanafunzi hao waliohitimu elimu ya msingi nchini kote. Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake kuendelea kielimu, na kukua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa kwani elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayostawi. “Natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kw...