BAADA ya Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kumsaka kwa siku mbili bila mafanikio mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu (CHADEMA), akidaiwa kumpiga na kumjeruhi mmoja wa askari wa Bunge, hatimaye alijisalimisha mwenyewe jana jioni. Taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni, Sugu alikwenda polisi akiongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki). Akizungumza na mwandishi wetu, Mnyika alisema kuwa Sugu hakukamatwa bali alijipeleka mwenyewe polisi kwa hiari yake na kwamba jioni hiyo majira ya saa 1:10 alikuwa akiandikisha maelezo yake. Wakati Sugu akijisalimisha, wanasheria wa Bunge nao walikuwa wamejifungia kuangalia namna ya kumkabidhi mbunge huyo mikononi mwa sheria. Juzi na jana viwanja vya Bunge vilitawaliwa na idadi kubwa ya polisi waliotumwa kumkamata Sugu lakini mpaka Bunge linaahirishwa jioni haikujulikana ni wapi alik...