Kafulila kuelezea sakata la Tegeta Escrow
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema ataanza kuelezea kwa kina sakata lililotikisa nchi la kashfa ya Tegeta Escrow wiki ijayo kupitia gazeti la Uwazi. Akizungmza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, Kafulila alisema amegundua kuwa kuna mambo mengi ambayo wananchi wanataka kuyajua kuhusu sakata hilo, hivyo ameamua kuyaandika yote ili kiu ya Watanzania kujua kuhusu sakata hilo iishe. “Najua kwamba mimi ndiye niliyelibebea bango bungeni sakata lile na kwa kuwa Gazeti la Uwazi linasomwa na watu wengi, nimeamua kuyaeleza yote kupitia gazeti hili kuanzia toleo lijalo,” alisema Kafulila. Alifafanua kuwa wazo la kuandika sakata hilo amelipata baada ya kuulizwa sana na baadhi ya wananchi kwamba liliishaje na jinsi lilivyomfanya akorofishane na vigogo wengi na hata kujihatarishia maisha. “Kwa kuwa hilo ni jambo zito, ni vema wananchi wajiandae kusoma kwa urefu juu ya sakata hilo kwenye gazeti hili. Nadhani nimefanya uamuzi sahihi,” alisema Kafulila.