Huwezi Kufanikiwa Penzini Bila ‘Mishale’, Ipokee Kadiri Uwezavyo!

UNAPO-MUONA mtu amefanikiwa kwenye uhusiano wake, amefunga ndoa na mwenza wake na kufanya sherehe, akili ya harakaharaka inaweza kukutuma uamini tu kwamba mambo ni rahisi tu.
Kwamba walikutana tu mahali fulani, wakakubaliana na kuanza safari ya urafiki, uchumba na mwisho wa siku wakaingia kwenye ndoa.
Bahati mbaya sana ni kwamba, unawakuta kwenye mafanikio. Unahisi pengine hawatumii nguvu nyingi kuendesha maisha yao na wanaelewana, hawagombani na kila uchwao wanafurahia maisha yao ya uhusiano.
Ndugu zangu, licha ya kwamba kila mtu ana historia yake na wapo ambao huingia kwenye ndoa bila kupitia changamoto nyingi, lakini kikubwa ninachoweza kukuhakikishia mimi ni kwamba, changamoto ni lazima uzipitie ili uweze kufikia malengo yako.
Tunafahamu kwamba kila mmoja anatamani aishi maisha mazuri yasiyokuwa na kelele, yasiyokuwa na misukosuko, lakini dunia ya wapendanao haipo hivyo. Mnakutana watu ambao hamjakua pamoja, mna tamaduni tofauti hivyo lazima mkumbane na changamoto za kutosha hadi mfikie hatua ya kuitwa mume na mke.
Penzi la kweli siku zote huwa linajengwa na historia. Lazima mpitie magumu na uwe tayari kuyavumilia kama kweli unataka kufika mbali. Hakuna njia ya mkato katika hili. Ukijaribu kuipita lazima utajikuta umeangukia pua.

Lazima ujue kwamba siku hazifanani. Kuna siku mwenzako anaweza akakasirika, kuna siku anaweza kuwa na furaha hivyo kama mwenzi wako, lazima uwe na uwezo wa kumsoma tabia na kujua namna ya kuishi naye kama mpenzi wako.
Kuna shida na raha. Kuna uzima na ugonjwa. Lazima ujifunze namna ya kuchuja taarifa, siyo umeambiwa tu kitu unakurupuka na kuanza kumsema vibaya mwenzako. Mwezako akipanda basi na wewe unapanda. Hakuna ambaye yupo tayari kumsikiliza mwenzake, mnapofikia hapo, jua kwamba safari yenu haiwezi kuwa na matokeo mazuri.
Mwenzako amekukosea, usikurupuke kufanya uamuzi maana wapo wanaofanya uamuzi wa haraka na kujikuta wanajutia mara tu baada ya kukaa na kutafakari vizuri juu ya uamuzi alioyafanya. Kama umejiridhisha kwamba upo na mtu sahihi, huna sababu ya kutangatanga.
Mvumilie mtu uliye naye, mheshimu mtu uliyekaa naye mwaka mmoja au miwili maana unamjua kuliko yule mpya utakayekwenda kukutana naye. Kubali kupokea changamoto mpya kila siku katika mapenzi maana siku hazifanani.
Mwenzako ana tabia fulani mbaya huipendi, mvumilie huku ukimpa elimu taratibu hadi atakapobadilika. Imetokea kweli mwenzako ameanguka, amefanya jambo ambalo linahatarisha uhusiano wenu, lipime kwa msamaha wake, halafu angalia kama anaweza kuuishi msamaha wake.
Maisha ya uhusiano wakati mwingine hayaishii tu kuwahusisha ninyi wawili, yanaunganisha pande zote mbili yaani ndugu wa mume na mke.
Wakati mwingine yawezekana ndugu wa upande fulani wakawa kikwazo cha uhusiano wenu, lakini usipaniki. Tumieni busara katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Yawezekana wazazi wakawa hawamtaki mtu uliye naye katika uhusiano, lakini busara zenu ndizo zitakazoamua muafaka wenu. Ninyi ndiyo mnaweza kuwashauri, kuwaeleza wazazi dhumuni lenu na umuhimu wa safari yenu.
Msiwe wepesi wa kukata tamaa, mtapingwa sana, mtakataliwa sana, lakini kama kweli mna nia ya dhati na mmemta-nguliza Mungu mbele katika safari yenu, hakika mtafanikiwa. Hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kukatisha safari yenu.
Watu wasiowatakia mema watasubiri muachane, lakini wapi, miaka itakatika ninyi mkiwa pamoja, mkifurahia maisha yenu katika shida na raha!

Comments

Popular posts from this blog