Rais John Magufuli amemuapisha Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Yakubu Hassan Mohamed. Luteni Jenerali Mohamed ameteuliwa jana Februari 14, 2018 kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na kupandishwa cheo kutoka Meja Jenerali na kuwa Luteni Jenerali. Luteni Jenerali Mohamed anachukua nafasi ya Luteni Jenerali, James Mwakibolwa ambaye amestaafu. Mbali na uteuzi huo, Rais Magufuli pia amewapandisha vyeo kutoka Brigedia Jenerali na kuwa Meja Jenerali J.G. Kingu, M.S. Busungu, R.R. Mrangira, B.K. Masanja, G.T. Msongole, A.F. Kapinga, K.P. Njelekela, A.S. Bahati, M.E. Mkingule na S.S. Makona. Taarifa ilitotolewa Ikulu jana imesema mabrigedia jenerali wote waliopandishwa vyeo watapangiwa vituo vya kazi baadaye. Kabla ya kuapishwa kwa Luteni Jenerali Mohamed, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo aliwavalisha vyeo mameja jenerali waliopandishwa vyeo na Rais Magufuli.