Wananchi Wamkataa Mkuu Wa Wilaya Mbele Ya Waziri Mkuu
WANANCHI
wa wilaya ya Kwimba wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na
mkuu wa wilaya hiyo Bw. Mtemi Msafiri baada ya kutoridhishwa na utendaji
wake.
Wametoa
ombi hilo jana (Ijumaa, Februari 16, 2018) walipozuia msafara wa Waziri
Mkuu alipowasili katika Ofisi za Halmashauri ya wilaya Kwimba zilizopo
Ngudu kwa ajili ya kuzungumza na watumishi akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoani Mwanza.
Wananchi
hao walimkataa mkuu wao wa wilaya Bw. Msafiri kupitia ujumbe wa mabango
17, ambapo Waziri Mkuu amewataka wananchi hao wawe watulivu wakati
Serikali inafanyia kazi malalamiko yao.
Wananchi
hao wanadai kwamba Mkuu huyo wa Wilaya anatabia ya kuamrisha polisi
wawakamate kwa kisingizio cha uzururaji na kisha wanawekwa mahabusu,
ambapo baada ya muda wanatolewa na kwenda kulima kwenye shamba lake.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inahitaji kila mtumishi atambue majukumu yake na
ayatekeleze. “Hakuna atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza nanyi
mnatakiwa kutenda haki kwa kuwatumikia wananchi.”
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mkuu huyo wa wilaya Bw. Msafiri,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba Bibi Pendo
Malebeja na wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli wanatekeleza
majukumu yao ipasavyo na kuwatumikia wananchi.
“Mkurugenzi
katika kipindi chako chote cha utendaji kuanzia mwaka 2013 hadi leo,
fedha nyingi za Serikali zilizoletwa Kwimba zimepotea na hazijulikani
zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika na muda wote huo Halmashauri
imekuwa inapata hati chafu.”
Pia
Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba
wabadilishe mienendo yao na wawatumikie vizuri wananchi pamoja na
kuishi nao vizuri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, FEBRUARI 16, 2018.
Comments
Post a Comment