Sababu za Faru Fausta kutumia Sh760 milioni kwa mwaka zatajwa
Arusha. Hakuna bosi yeyote serikalini anayelipwa zaidi ya Sh17 milioni baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kutekeleza sera zake za kubana matumizi, lakini yupo kiumbe hai mmoja tu ambaye matumizi yake yalifika Sh64 milioni kwa mwezi; na kuna sababu za kuhalalisha gharama hizo. Kiumbe huyo ni mnyama mwitu aina ya faru aliyepewa jina la Fausta, ambaye sasa anatumia Sh20.4 milioni. Fausta ndiye faru kikongwe kuliko wote nchini, akiwa na umri wa miaka 54, na anahitaji matunzo mazuri ili aendelee kuvuta watalii na wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia. Fausta anaishi Hifadhi ya Ngorongoro ambako analindwa kwa saa 24 kumuepusha kushambuliwa na wanyama wengine kama fisi na mbwa mwitu kutokana na uzee, lakini gharama za ulinzi zitapungua baada ya kupata makazi salama ndani ya mwitu jengo lake litakapomalizika. Hiyo ni sehemu tu ya gharama zinazomfanya Fausta kutumia fedha nyingi zaidi ya mfanyakazi mwandamizi wa serikalini. Kazi ipo kwe