Mbunge wa Mbeya maarufu kwa jina la SUGU ajisalimisha polisi baada ya kutafutwa kwa siku mbili


BAADA ya Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kumsaka kwa siku mbili bila mafanikio mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu (CHADEMA), akidaiwa kumpiga na kumjeruhi mmoja wa askari wa Bunge, hatimaye alijisalimisha mwenyewe jana jioni.

Taarifa zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni, Sugu alikwenda polisi akiongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki).

Akizungumza na  mwandishi wetu, Mnyika alisema kuwa Sugu hakukamatwa bali alijipeleka mwenyewe polisi kwa hiari yake na kwamba jioni hiyo majira ya saa 1:10 alikuwa akiandikisha maelezo yake.

Wakati Sugu akijisalimisha, wanasheria wa Bunge nao walikuwa wamejifungia kuangalia namna ya kumkabidhi mbunge huyo mikononi mwa sheria.

Juzi na jana viwanja vya Bunge vilitawaliwa na idadi kubwa ya polisi waliotumwa kumkamata Sugu lakini mpaka Bunge linaahirishwa jioni haikujulikana ni wapi alikokuwa mbunge huyo.

Mbunge huyo juzi baada ya kubebwa mzobemzobe na askari wa Bunge na kisha kutolewa nje ya ukumbi, inadaiwa kuwa alimpiga ngumi mmoja wa askari aliyemtuhumu kuwa alikuwa amempia ngumi wakati wakimtoka nje.

Askari hao juzi jioni walikuwa kwenye vikundi vikundi nje ya ukumbi wa Pius Msekwa ambako kulikuwa kukifanyika mkutano wa wabunge wa upinzani ambapo Sugu pia alikuwa miongoni mwao.

Kutokamatwa kwa Sugu kumewashangaza wengi waliokuwa karibu na askari hao kwa kuwa alikuwa amekaa jirani nao akizungumza na wenzake kabla ya kuanza kwa kikao chao.

Tanzania Daima lilidokezwa kuwa askari hao walishindwa kumkamata Sugu kwa kuwa hapakuwepo na amri ya kukamatwa kwake na hata ilipotolewa alikuwa ameshaondoka katika viwanja vya Bunge.

Mpaka Bunge linaahirishwa juzi jioni, idadi kubwa ya askari walikuwa nje ya milango na korido zilipo ofisi za kambi ya upinzani wakimsubiri Sugu bila mafanikio.

Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia askari kusuasua kukamatwa kwa Sugu ni kutokana na kinga ya kibunge aliyonayo na pia kosa analotuhumiwa kulifanya alilifanya akiwa kwenye viwanja vya Bunge.

“Tulipata mtanziko wa kumkamata haraka haraka, ilibidi lazima tuwasiliane na ofisi ya Spika kujua taratibu za kumkamata kiongozi huyo hasa kwa kuwa alifanya kosa hilo akiwa bungeni,” kilisema chanzo kimoja.

Wakati askari wakihaha kumtafuta Sugu, mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), jana aliomba mwongozo wa Spika kuhusu tukio la vurugu zilizotokea juzi bungeni hasa tukio la Sugu kumpiga askari.

Sendeka alisema tukio hilo limelidhalilisha Bunge na askari wanaowalinda, hivyo akataka liweke wazi ni hatua gani zitakazochukuliwa dhidi ya mbunge huyo ili kulinda heshima ya chombo hicho.

“Nataka nijue ibara ya 100 ambayo humpa kinga mbunge na uhuru wa mawazo akiwa ndani ya Bunge inatumikaje katika tukio hili?

“Je, Bunge litalindaje heshima yake dhidi ya tukio hili lililofanywa na mbunge mwenzetu?” alihoji.

Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema tukio hilo ni geni hivyo Bunge limeshindwa kutoa jibu la mara moja.

“Jambo hili halijawahi kutokea katika historia ya Bunge, sasa nami nitalifikisha kwa wanasheria wa Bunge wanishauri namna ya kulishughulikia na baada ya hapo nitatoa mwongozo,” alisema.

Akitoa mwongozo huo muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa jana jioni, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kuwa bado wanashauriana na wanasheria kuona kanuni zinawaelekezaje.

Alisema kuwa licha ya tukio hilo kutokea katika eneo la Bunge bado kitendo hicho ni cha jinai na hivyo, mtuhumiwa atashughulikiwa kisheria.

“Ni sawa na jaji yuko mahakamani ambapo kuna kinga kama za Bunge halafu jaji mwenzake ampige ngumi. Huyo lazima achukuliwe hatua hawezi kuachwa. Kinga zetu ziko kwenye uhuru wa mawazo tu,” alisema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, juzi lilitangaza kumsaka Sugu kwa tuhuma za kufanya vurugu na kumjeruhi askari wa Bunge.
 
“Lakini tuna mashaka sana na hatua yake aliyoifanya nje ya ukumbi ambapo alimvamia na kumpiga ngumi nzito Koplo Nikwisa Nkisu ambaye alijeruhiwa jicho,” alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Dodoma ASP Jumanne Kim, juzi jioni alithibitisha kusakwa kwa mbunge huyo aliyeondoka maeneo ya Bunge mchana akiwa ndani ya gari la kiongozi mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe.

Comments

Popular posts from this blog