MAKAMBA AVUNJA REKODI YA MAPOKEZI NA UDHAMINI IRINGA

Wanafunzi wa Iringa University wakimpokea Mhe. Makamba kwa shangwe na furaha huku wakiwa wameshika mabango
Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia anayeendelea kusaka udhamini wa wananchama wenzake  ili kuingia katika kinyang’anyiro cha Urais mapema Oktoba mwaka huu, Mheshimiwa January Makamba, leo amepokelewa kwa kishindo na wanachama wa CCM Mjini Iringa na kuvunja rekodi ya udhamini ukilinganisha na wagombea waliopita.
Akiongea kabla ya kumkaribisha mtangaza nia huyo anayeonekana kuwa na mvuto wa aina yake kwa vijana, Katibu wa CCM wilaya ya Iringa Zongo Lobe Zongo amemtaja Mheshimiwa Makamba kuwa ni mgombea aliyevunja rekodi mkoani hapo baada ya kupata wadhamini 680 ukiachilia mbali mapokezi yenye msisimko mkubwa tofauti na wagombea waliotangulia.
Akiwashukuru Mheshimiwa January Makamba, ambaye anaomba kupendekezwa na chama chake kugombea nafasi ya urais, alisema kwamba ameamua kugombea si kwa kubip bali anagombea kushinda, pia kwamba hagombei kupambana na mtu yeyote bali anagombea kupambana na changamoto za wananchi.
Mheshimiwa Makamba, amewahakikishia wanachama wa CCM wa Iringa kwamba akifanikiwa kuteuliwa na chama chake kugombea urais wa taifa letu, atahakikisha jimbo la Iringa mjini linarudi CCM. Pia kwamba atahakikisha viwanda vyote vya Iringa vilivyokuwa vikifanya kazi zamani vinafufuliwa. Pia kwamba uwanja wa ndege wa Iringa utaboreshwa ili kuruhusu ndege kubwa kutua.
Mheshimiwa Makamba, amewakumbusha wanachama wa CCM Iringa kwamba yeye atayashughulikia makundi yote, vijana, wanawake na wazee. Vijana wa boda boda atahakikisha wanaondokana na  kufanya kazi kwa kuwatumikia wengine, na watawezeshwa ili kumiliki pikipiki zao wenyewe.

Comments

Popular posts from this blog