SHEHA ALIYEKUTWA NA BANGI ATIMULIWA KAZINI HUKO UNGUJA
SERIKALI katika mkoa wa Kusini Unguja, imemtimua kazi Sheha wa Kitumba, Mtwana Kificho, ambaye wiki iliyopita nyumbani kwake alikutwa na majani makavu yanayosadikiwa kuwa bangi baada ya polisi kufanya ukaguzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Dk Idrissa Muslim Hijja, jana aliwateuwa masheha wawili na kuwaapisha kuongoza shehia hizo, pamoja na sheha mpya wa Kitumba, Makame Chum.
Akizungumza na masheha hao katika eneo
la Tunguu katika mkoa wa Kusini Unguja, Dk Hijaa, aliwataka masheha hao
kutekeleza majukumu yao ya kuongoza kwa busara katika maeneo yao kwa
mujibu wa sheria.
Alisema masheha ni watendaji na
wasimamizi wa majukumu ya wananchi, ambapo matatizo yao wanatakiwa
kuwasilishwa mbele ya Serikali Kuu kupatiwa ufumbuzi.
“Majukumu ya kazi kwa masheha ni
kusimamia matatizo ya wananchi na kuyaelekeza kwa Serikali Kuu kwa ajili
ya kupatiwa ufumbuzi na sio kuchochea mifarakano katika jamii,”
alisema.
Kwa mfano Mkuu wa Mkoa aliwataka masheha
hao kuacha kujiingiza katika migogoro ya ardhi na mashamba ya wananchi
katika sehemu zao. Alisema Serikali imepiga marufuku masheha kujiingiza
katika migogoro ya ardhi pamoja na kuuza mashamba ya wananchi.
“Serikali imepiga marufuku masheha
kujiingiza katika migogoro ya ardhi na kuuza mashamba ya
wananchi...sheha atakayebainika kufanya vitendo hivyo, atachukuliwa
hatua za kinidhamu,” alisema.
Malalamiko makubwa ya wananchi wa
Kitumba wilaya ya Kati Unguja ni wizi wa mazao kwa wakulima, pamoja na
mifugo na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya kilimo.
Masheha waliokula kiapo mbele ya Mkuu wa
Mkoa ni Makame Chum kuongoza shehia ya Kitumba na Foum Ali Foum, shehia
ya Marumbi wilaya ya Kati.
Akizungumza katika sherehe fupi mara
baada ya kula kiapo, Foum alisema atahakikisha anayapatia ufumbuzi na
kuyashughulikia matatizo yanayowakabili wananchi wa eneo lake, ikiwemo
kupambana na uvuvi haramu.
“Katika shehia ya Marumbi, tunakabiliwa
na tatizo moja la uvuvi haramu ambalo nimekusudia kulifanyia kazi kwa
karibu zaidi na kuishauri Serikali kadri ya matatizo yanavyojitokeza,”
alisema.
Comments
Post a Comment