RAIS MAGUFULI ATUMBUA VIGOGO 300 KWA UOZO NDANI YA SERIKALI
RAIS
Dk. John Magufuli anaelekea kufunga mwaka huku akiwa amesafisha
Serikali yake ya awamu ya tano kwa kuwatumbua watendaji zaidi ya 300
tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana.
Hatua
hiyo imekuja baada ya kubainika uozo ndani ya Serikali, huku baadhi ya
watendaji wa ngazi za juu wakihusishwa na tuhuma mbalimbali, ikiwamo za
matumizi mabaya ya ofisi na ufisadi.
Hatua
hiyo inaelezwa ni miongoni mwa mkakati wa kuzika mfumo wa Serikali ya
awamu ya nne ambao baadhi ya vigogo walikuwa wakifanya mambo holela na
kusahau wajibu wao kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Uchukuaji
huo wa nidhamu kwa idadi kubwa ya watumishi wa Serikali, inaonyesha
kuwa kila siku kuna wastani wa kigogo mmoja mtendaji wa juu ambaye
amejikuta akifutwa kazi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutumia madaraka
vibaya na kuisababishia hasara Serikali.
Fagio
hilo linajumuisha watumishi wa Serikali waliosimamishwa kazi kutoka
taasisi mbalimbali na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa.
Asilimia
kubwa ya vigogo waliosimamishwa kazi walichukuliwa hatua na Rais
mwenyewe na wengine Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, huku wawili
wakiwajibishwa na mawaziri husika katika wizara wanazoongoza.
Tukio la
hivi karibuni, kiongozi huyo wa nchi alitengeua uteuzi wa aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu
(NIMR), Dk. Mwele Malecela, ambaye alitangaza utafiti wa ulioonyesha
uwapo wa ugonjwa wa Zika nchini.
Dk. Mwele alisema utafiti huo ulifanywa na NIMR kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Bugando (Cuhas).
Siku moja
baada ya kutenguliwa kwa kigogo huyo, Rais Magufuli alimtangaza
aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Yunis
Mgaya kuwa mrithi wa nafasi hiyo.
WALIOTUMBULIWA
Wengine
ambao waliondolewa kwenye nafasi zao na hata kujikuta wakifikishwa
kortini ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA), Dickson Maimu na wenzake wanne.
Mbali na
Maimu, wengine waliotumbuliwa ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani,
Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na
Ofisa usafirishaji, George Ntalima.
Januari
15, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kufuta uteuzi wa aliyekuwa
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk. Feisail Issa, ambaye ilidaiwa alitaka
kupigana na Mkuu wa mkoa huo, Magesa Mulongo.
MADENI KIPANDE
Januari
25, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa Madeni
Kipande kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa
Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Taarifa
iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Balozi Ombeni
Sefue, ilisema uteuzi wa Kipande umetenguliwa kabla muda wake wa
majaribio haujaisha wa miezi sita, kwa vile amebainika kuwa na utendaji
mbovu.
Kipande
alihamishiwa Mkoa wa Katavi baada ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta, kumsimamisha kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
ambako alikuwa Mkurugenzi Mkuu. Alisimamishwa kutokana na tuhuma
mbalimbali za ubadhirifu.
KIRANJA WA MAKATIBU WAKUU
Machi 6,
mwaka huu Rais Magufuli, alitangaza kumng’oa aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Sefue kuhudumu katika wadhifa huo, Ikulu Dar es Salaam.
Balozi Sefue amehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 65 tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana.
Hatua
hiyo ya kuondolewa katika nafasi hiyo ya kiranja wa makatibu wakuu wa
wizara, ilikuja siku chache baada ya gazeti moja la wiki kuripoti juu ya
kashfa na kumuhusisha Balozi Sefue na ufisadi katika miradi kadhaa ya
maendeleo.
MA-RC
Machi 13,
mwaka huu mkuu huyo wa nchi aliwaweka kando wakuu wa mikoa 13 baada ya
kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo kati yao 13
ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa vituo
vya kazi na mmoja alipangiwa Mkoa mpya wa Songwe.
WAZIRI MAMBO YA NDANI
Machi 20, mwaka huu Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Rais
Magufuli alitengua uteuzi huo kutokana na kitendo cha Kitwanga kuingia
bungeni na kujibu swali linaloihusu wizara yake akiwa amelewa.
Aprili
26, mwaka huu Rais Magufuli alivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk.
Ally Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa
mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS) na kusababisha nchi
kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Machi 22,
2013 TCRA iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji
na uhamishaji wa mapato ya simu. Kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza
vipengele vitano, lakini hadi wakti huo ilikuwa haijaanza kutekeleza
kipengele kidogo kinachohusu udhibiti wa mapato ya simu za ndani
(Offnet).
MAKATIBU TAWALA
Aprili
26, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza uteuzi wa makatibu tawala wa
mikoa 26, akiwatoa 10 wa zamani na kuingiza wapya, wawili
wakibadilishiwa vituo vyao vya kazi, huku 13 wakibakishwa katika vituo
vyao.
Mei 25,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, alitangaza kuvunja uongozi wa
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuwapumzisha kutekeleza majukumu yao Katibu
Mtendaji, Profesa Yunus Mgaya, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose
Kiishweko, Mkurugenzi wa Ithibati, Dk. Savinus Maronga na Ofisa
Mwandamizi wa Takwimu, Stambuli Kimboka.
Mbali na hilo, hivi karibu ilitangazwa kutumbuliwa kwa vigogo watatu wa Taasisi ya Elimu (TEA).
WAKURUGENZI 120 NJE
Julai 7,
mwaka huu, Rais Magufuli aliwaweka kando wakurugenzi 120 alipofanya
uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji matano, manispaa 21, miji
22 na wilaya 137 za Tanzania Bara.
Uteuzi huo ulitangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Mussa Iyombe.
Kati ya wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 wameteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya.
MA-DAS 40 WAACHWA
Julai 6,
mwaka huu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, ilitangaza kujaza nafasi zilizokuwa wazi za Ma-DAS katika Wilaya
mbalimbali. Nafasi hizi zimetokana na kustaafu, kufariki na wengine
kupoteza sifa za kuendelea katika nafasi hiyo.
Kutokana na orodha hiyo, Ma-DAS wa zamani 40 walipoteza nafasi, huku wapya wakichanua katika uteuzi huo.
WAKURUGENZI ATCL
Novemba
mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso,
alitangaza uamuzi wa bodi wa kuwaengua wakurugenzi watano waliokuwa
katika idara mbalimbali, ikiwamo ya biashara, ambayo ilikuwa na kaimu.
Wakurugenzi walioondolewa ni fedha, usalama, ufundi na uendeshaji, ambayo mkurugenzi wake alikuwa anaelekea kustaafu.
WAZIRI AFYEKA WATANO TASAF
Katika
kile kinachoonekana kusimamia utendaji wa Serikali ya awamu ya tano kwa
kupinga ufisadi, Desemba 5, mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki,
alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf),
kuwasimamisha kazi maofisa waandamizi watano wa mfuko huo.
Maofisa
hao ni wanaosimamia mpango huo pamoja na Meneja wa Uratibu na Mkurugenzi
wa Uratibu kutokana na kushindwa kusimamia mpango wa kunusuru kaya
masikini.
Kairuki
alisema maofisa hao ndio viongozi wasimamizi wakuu wa mpango huo katika
Awamu ya Tatu ya Tasaf na wamesimamishwa kupisha uchunguzi wa jinsi
walivyohusika kuvuruga utekelezaji wa mpango huo hadi kufikia
kuandikisha kaya zisizo na sifa.
Kairuki
alisema ameshauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na tayari ameshaelekeza waratibu wa
Tasaf 106 wa wilaya pia wasimamishwe kazi.
MSAJILI WA HAZINA
Desemba
7, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza uamuzi mgumu wa kufuta uteuzi wa
aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, ambaye alielezwa
atapangiwa majukumu mengine.
MAKATIBU WAKUU
Desemba
30, mwaka jana, Rais Magufuli aliwatema makatibu wakuu wa zamani watano
katika uteuzi wake, ambao ni Dk. Donald Mbando (Afya), Balozi Liberata
Mulamula (Mambo ya Nje), Omari Chambo (Nishati na Madini), Jumanne
Sagini (Tamisemi) na Joyce Mapunjo (Wizara ya Afrika Mashariki).
Januari
25, mwaka huu aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba
yao imeisha.
Aliwataja
mabalozi hao kuwa Dk. Batilda Salha Buriani, aliyeko Tokyo nchini Japan
na Dk. James Msekela, aliyekuwa Rome, Italia ambaye hivi karibuni
ameteuliwa tena kuwa balozi.
Rais
Magufuli, pia alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyekuwa London,
Uingereza, Peter Kallaghe, ambaye alirudishwa Wizara ya Mambo ya Nje,
Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ambako ilielezwa
kuwa atapangiwa kazi nyingine. Sasa ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nchi
katika Chuo cha Jeshi Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilisababisha kuwa na vituo sita vya balozi za Tanzania ambavyo vimeachwa wazi.
Vituo
hivyo ni London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Kallaghe, Brussels
Ubelgiji, kufuatia aliyekuwa Balozi Kamala kuchaguliwa kuwa mbunge na
Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dk. Msekela.
Wengine
waliosimamisha kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani
ya Ocean Road, Dk. Diwani Msemo, huku Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi
Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Asteria Mlambo naye akijikuta
akiwekwa kando.
Rais
Magufuli, alitangaza pia kufuta uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhadard
Tito, na kuvunja bodi yake sambamba na ile ya Kampuni ya Reli Tanzania
(TRL).
VIGOGO NSSF
Julai 18,
mwaka huu vigogo sita ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Taifa la
Hifadhi za Jamii (NSSF), makao makuu jijini Dar es Salaam, wakiwamo
mameneja wengine watano, walisimamishwa kazi.
Wakurugenzi
hao walisimamishwa ili kupisha uchunguzi, ambao hadi sasa haijajulikana
hatima yao baada ya Bodi ya Wadhamini ya Shirika hilo kukutana Julai 15
mwaka huu, chini ya mwenyekiti wake Profesa Samwel Wangwe.
Viongozi
hao, walisimamishwa kupisha uchunguzi kubaini wahusika katika tuhuma za
ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na
taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na
ajira.
Waliosimamishwa
ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula,
Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na
Utawala, Chiku Matessa, Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga, Sadi
Shemliwa, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani, Pauline Mtunda na
Mkurugenzi wa Uendeshaji, Crescentius Magori.
Mbali na
hao pia wapo mameneja waliosimamishwa ambao ni Meneja wa Utawala, Amina
Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli, Meneja wa Miradi,
mhandisi John Msemo, Mhasibu Mkuu, Davis Kalanje, Meneja Kiongozi, Mkoa
wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na Mhandisi John Ndazi ambaye ni
Meneja Miradi.
Wakati
hali ikiwa hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli,
alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dk.
Ramadhan Dau na kumteua kuwa balozi ambaye sasa yupo nchini Malaysia.
Baada ya
mabadiliko hayo, mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama, alimteua Dk. Carine Wangwe kuwa Mkurugenzi mkuu mpya
wa shirika hilo.
Hata hivyo, saa chache baada ya uteuzi huo, Ikulu ilitengua uteuzi huo kwa kile kilichoelezwa kuwa haukufuata utaratibu.
MUHIMBILI
Novemba
9, 2015, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili na kukuta Mashine ya MRI na CT-Scan hazifanyi kazi jambo
lililomfanya avunje bodi ya wadhamini ya hospitali hiyo iliyokuwa na
wajumbe 11.
Mbali na
kuvunja bodi hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Dk. Hussein Kidanto
aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi wa hospitali hiyo na kumrudisha
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jami.
BANDARINI
Novemba
27, 2015 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza
Bandari ya Dar es Salaam, na kubaini kuwa makontena 329 yalitolewa
bandarini bila kulipiwa kodi na kusababishia Serikali hasara ya Sh
bilioni 80.
Kati ya
waliowekwa pembeni, maofisa walikuwa 12 na wengine wakiwa ni wajumbe wa
bodi iliyovunjwa huku akitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka.
TAKUKURU
Desemba
16, mwaka jana Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea,
kwa kile kilichoelezwa kuwa alijiridhisha kuwa alishindwa kushughulikia
rushwa kwenye bandari ya Dar es Salaam.
TANESCO
Desemba
6, 2015, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilisimamisha maofisa saba
kwa kile kilichodaiwa kwamba ni kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo
wizi na ubadhirifu.
Chanzo-Mtanzania
Comments
Post a Comment