Mwanafunzi akipata mimba mzazi jela miaka 30
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa wazazi wote wawili wa mtoto wa kike atakayekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa ama akipata ujauzito. Aidha amesema Serikali itamfunga jela miaka 30 kijana anayetaka kumuoa msichana anayesoma pamoja na wazazi wake. Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumlinda mtoto wa kike katika kuhakikisha kuwa anapata haki yake ya msingi ya kusoma kufikia elimu ya chuo kikuu kwa kujenga mabweni na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaowapa mimba na kuwaozesha katika umri mdogo na kukatisha masomo yao. Majaliwa aliyasema hayo jana wilayani Hanang, mkoani Manyara katika ziara yake ya kikazi ya siku sita kwa mkoa huo. Alisisitiza kuwa kupitia sera ya kuboresha elimu nchini serikali imeondoa michango ya fedha za kulipia bili za maji, umeme, gharama za mlinzi na mitihani ili kumpunguzia gharama mzazi na mlezi na kuwaacha wazazi kushughulikia maeneo mengine muhimu