BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA), limeifungia video ya wimbo ‘Nimevurugwa’ ya mkali wa muziki wa mduara, Snura Mushi ‘Snura’ kwa madai ya kukosa vigezo vya kimaadili kwa jamii. Akizungumza hivi karibuni, Snura alisema hajui ni sababu gani iliyofanya kazi yake kufungiwa kupigwa katika vituo vya televisheni. “Nilipigiwa simu na rafiki zangu na kuambiwa hivyo, lakini mpaka sasa sijui ni kwa sababu gani maana sioni kama nimefanya kitu cha ajabu katika video hiyo na cha kushangaza hata sijaulizwa na yeyote, ila ndiyo hivyo,” alisema. Snura alisema wakati amesambaza video ya wimbo wake ‘Majanga’, kuna baadhi ya mashabiki walimshangaa ni kwanini hajacheza katika kazi hiyo kitu kilichosababisha video ya wimbo huo kupooza na kutokuwa na mvuto kwa mashabiki wake. “Nilivyopata malalamiko hayo, nikaona nisiwaboe kwa kuendelea kutoa video ambazo sichezi. Katika wimbo uliofuata nikacheza, kumbe nilikuwa naandaa mazingira ya kufungiwa,” alisema. Snura ...