Haya ni Matokeo ya Mtihani wa darasa la saba 2013
Imeelezwa kuwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mwaka 2013 umepanda kwa masomo yote kwa asilimia 19.89 ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka uliopita. Kwamba, wakati mwaka jana wahitimu waliopata asilimia 100 walikuwa asilimia 30.72, mwaka huu wameongezeka kuwa asilimia 50.61. Pia, somo ambalo watahiniwa hao wamefaulu zaidi katika mtihani wao ni Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 69.06 huku wakiwa wamefeli zaidi kwenye somo la Hisabati ambalo ufaulu upo chini kwa asilimia 28.62. Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 427,606 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 huku kiwango cha udanganyifu kikizidi kudhibitiwa hivyo kupungua. Alisema NECTA imefuta matokeo yote ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa 13, ambao walibainika kufanya udanganyifu kwenye mtihani au kurudia pasipo ruhusa ya Baraza. Watahiniwa waliofutiwa mwaka jana ni 293.