Polisi: Tutamkamata na Kumhoji Askofu Kakobe kwa Uchochezi
Licha
ya kutokiri moja kwa moja juu ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu
kumkamata Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship (FGFC) lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi
limesema ni lazima litamhoji kiongozi huyo wa kiroho.
Kuhojiwa huko kumetokana na kauli yake dhidi ya serikali aliyoitoa wakati wa ibada ya Krismasi.
Jana, kulienea taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii
kueleza kwamba askofu huyo alitiwa mbaroni jana asubuhi na askari wa
Jeshi la Polisi huku sababu za kukamatwa zikielezwa kuwa ni ujumbe
alioutoa wakati wa mahubiri yake ya ibada ya Krismasi.
Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na ukweli wa taarifa za
kutiwa mbaroni kwa Askofu Kakobe, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar
es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa ni kweli walishakuwa katika
harakati za kumkamata.
“Ametoa maneno ya kashfa katika mahubiri yake, lakini sina taarifa kama amekamatwa,” Kamanda Mambosasa alisema na kuongeza:
“Taarifa za kumkamata zipo, lazima tumkamate. Tutamhoji…tutamhoji alikuwa na maana gani.
“Mtu akitenda kosa la jinai ni lazima akamatwe…kwa sasa niko
msibani, sijapokea taarifa kama amekamatwa au kuhojiwa. Nitawaarifu kama
kutakuwa na taarifa zaidi.”
Askofu Kakobe (62), anadaiwa kuyatumia mahubiri yake siku hiyo
kuzungumzia mwenendo wa serikali na masuala mbalimbali ya kisiasa
nchini.
Mojawapo ya sauti inayodaiwa kuwa ya Askofu Kakobe na kusambaa
kwenye mitandao ya kijamii ilidai kwamba hivi sasa Tanzania si nchi ya
chama kimoja kama viongozi wanavyotaka.
Chanzo: Nipashe.
Comments
Post a Comment