NYUMBA ALIMOFICHWA ‘MO’ YAFAHAMIKA, NI MBEZI BEACH DAR
NYUMBA inayodaiwa kuwa ndimo alifichwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ baada ya kutekwa na watu ambao bado hawajajulikana hadi leo ipo eneo la Mbezi-Beach jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, ameonyesha nyumba hiyo ambayo watekaji hao waliikodisha kwa kupanga kwa kusaidiwa na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Twalib Mussa.Kwa mujibu wa maelezo ya Mambosasa, kufuatana na uchunguzi uliofanywa kwa kumhusisha pia Twalibu, watekaji hao walitoka Afrika Kusini.
Mambosasa alisema kupatikana kwa nyumba ambayo ilikuwa inamilikiwa na mtu mmoja marehemu aliyemtaja kwa jina la Mwansasu, ni moja ya hatua muhimu katika sakata hilo lililoanza kwa kutekwa kwa mfanyabiashara huyo kijana siku ya Oktoba 11 mwaka huu ambapo leo umetimia mwezi hadi kupatikana kwa nyumba aliyokuwa ametunzwa.
Akifafanua zaidi, Mambomsasa, alisema Twalibu ambaye ni dereva wa teksi na mwenyeji wa Tanga pamoja na kuwasaidia kupanga katika nyumba hiyo, ndiye aliyewasafirisha kutoka eneo watekaji walipomwacha Mo, viwaja vya Gymkhana, na kuwapeleka hadi kituo cha mabasi cha Ubungo ambako wanasemekana waliondoka na kwenda kusikojulikana.
Gari alilotumia Twalibu kuwasafirisha watu hao lina namba za usajili za T918 CCY.
Comments
Post a Comment