TFF Yapangua Kikosi Cha Simba

Kikosi cha timu ya Simba SC.

KIKOSI cha Simba ambacho kitashuka dimbani kesho kumenyana na Stand United kitakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na sababu mbalimbali.
Simba, kesho Jumapili itakuwa Uwanja wa Taifa kusaka alama tatu muhimu mbele ya Stand United.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems amelazimika kukifanyia mabadiliko kikosi chake hicho kutokana na baadhi ya wachezaji wake kukumbana na adhabu mbalimbali kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mabadiliko hayo ya kikosi cha Simba yanahusika zaidi kwenye safu ya ulinzi ambapo nyota wake wawili James Kotei na Erasto Nyoni wataukosa mchezo huo kutokana na kufungiwa na TFF.

Wachezaji hao walibainika walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu. Pia Simba itamkosa nahodha wake, John Bocco ambaye naye alikumbwa na adhabu hiyo. Kiungo Jonas Mkude anaweza kukosekana kutokana na kuwa majeruhi.
Aussems ameliambia Championi Jumamosi kuwa, kutokana na hali hiyo amelazimika kukifanyia mabadiliko kikosi hicho kwa kuwaanzisha baadhi ya wachezaji ambao katika mechi zilizopita walikuwa wakianzia benchi.

“Sina jinsi imenibidi nifanye hivyo, lakini wachezaji wangu wote wapo vizuri na ninaamini watakaochukua nafasi hizo watacheza kwa kiwango cha juu.

“Tunahitaji kupata pointi tatu mbele ya Stand timu inapitia katika kipindi kigumu lakini kupambana ni jambo la muhimu kwetu na hatuna muda wa kupoteza ni lazima tufanya vizuri sasa na si wakati mwingine,” alisema Aussems.

Wachezaji ambao wanatarajia kuchukua nafasi za wachezaji hao ni Mzamiru Yasini atakayecheza nafasi ya Kotei, Said Ndemla yeye atakuwa mbadala wa Mkude, mlinzi Paul Bukaba atachukua nafasi ya Nyoni wakati Adam Salamba atacheza badala ya Bocco.

Hata hivyo, katika mazoezi ya juzi na jana jioni, Aussems alikuwa akiwafua vilivyo wachezaji hao ili kuhakikisha wanakuwa fiti na tayari kwa mchezo huo.

Wakati huohuo wachezaji wa kimataifa, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid kutoka Uganda pamoja na Mzambia Claytous Chama jana walianza mazoezi baada ya kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa huku Mrwanda Haruna Niyonzima akitarajiwa kutua Jumatatu.
Stori: Sweetbert Lukonge na Martha Mboma

Comments

Popular posts from this blog