KUVISHWA PETE YA UCHUMBA, SIRI 3 KILIO CHA LULU ZAFICHUKA

Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuvishwa pete ya uchumba na Francis Shiza ‘Majizo
BAADA ya wikiendi iliyopita staa ‘grade one’ wa filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuvishwa pete ya uchumba na bosi wa Radio EFM, Francis Shiza ‘Majizo’ na kuangua kilio cha aina yake, siri tatu (3) zimefichuka, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.

Kwa mujibu wa mtu aliyehudhuria, shughuli hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Majizo, Mbezi-Beach jijini Dar ilikuwa ya aina yake kwani watu walifurahi kwa kula na kunywa huku mastaa wa filamu wakionekana kutoalikwa au kutokuwepo.

“Unajua ishu ya Lulu kuvishwa pete ya uchumba ilikuwa ni siri sana ndiyo maana hakukuwa hata na mastaa wenzake wa filamu zaidi ya mwigizaji Mahsein Awadhi ‘Dk Cheni’ ambaye alikuwa mshehereshaji lakini ilifana kwani mpaka Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda alikuwepo,” alieleza mtu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.

SHEREHE ILIKUWA HIVI
Chanzo kiliendelea kutiririka kwamba sherehe ilianza vizuri na wakati ulipofika wa bosi huyo wa radio kumvisha pete Lulu, alipiga magoti na kushika mkono wa msanii huyo kwa ajili ya kumvisha.
Cha kushangaza, ile Majizo anamshika tu Lulu mkono, mwanadada huyo alianza kuangua kilio kama chote mpaka anamaliza kuvishwa kisha wakakumbatiana na bosi huyo kuwa na kazi ya ziada ya kumbembeleza mchumba’ke huyo.

SIRI TATU ZATAJWA
Kutokana na kuangua kilio huko, siri tatu za mwanadada huyo kulia zilitajwa ambazo ni kama ifuatavyo;
1: MAPITO
Lulu alionekana kulia sana kutokana na mapito aliyoyapitia kwani kwa umri alionao amepitia mambo makubwa zaidi ya uwezo wake ikiwa ni pamoja na kesi ambayo bado anatumikia kifungo cha nje ile inayohusiana na kifo cha aliyekuwa msanii maarufu wa filamu, marehemu Steven Kanumba. Aprili 7, 2012, Lulu aliibua mshtuko baada ya kudaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia huku akiwa ndiye mchumba wake wa awali.

Katika mapito yake ya kutaka kuolewa ikashindikana, awali alikuwa aolewe na Kanumba, lakini mpango huo ulishindikana baada ya jamaa huyo kufariki dunia. Hata hivyo, mwaka 2015, zilivuja habari za Lulu kupata mchumba ambaye ni Majizo, lakini kila alipoulizwa alikanusha habari hizo.
Mwaka 2016 zilivuja habari mbaya kuwa uchumba huo uliingia dosari na kuvunjika kabla ya kuimarika tena mwaka 2017. Alipoulizwa Lulu kama ana neno lolote kwa Majizo alisema: “Namshukuru kwa kunichagua mimi kati ya wengi.”

2: KUSHINDA MIONGONI MWA WANAWAKE WENGI
Ilifahamika kuwa sababu ya pili ya kulia ni kutokana na uwepo wa wanawake wengi wazuri na kila siku wanazaliwa, lakini Lulu amekuwa mmojawapo mwenye bahati kwani mchumba wake huyo aliwaona hao wengi ila akaamua kumchagua yeye. Mbali na Lulu, Majizo aliwahi kuwa na wanawake wengine akiwemo mwanamitindo Hamisa Mobeto, lakini akaamua kumchumbia Lulu hivyo mwanadada huyo hakuwa na budi kuangua kilio.

3: FURAHA
Siri nyingine ni kwamba Lulu aliangua kilio kutokana na furaha iliyopitiliza aliyokuwa nayo kwani kwa mujibu wake hakutarajia kama atavishwa pete na mchumba wake huyo na wala alikuwa hajui chochote. Machozi mengine yalitokana na kuona ndoto yake ya kuolewa na Majizo inaenda kukamilika hivyo ile furaha ndiyo ikageuka kilio.

MAMA KANUMBA AKUBALI YAISHE
Baada ya tukio la kuvishwa pete kwa Lulu, gazeti hili lilizungumza na mama wa marehemu Kanumba ambaye enzi za uhai wa mwanaye alikuwa mkwewe, Flora Mtegoa ambaye alifunguka na kutoa kauli ya kukubali yaishe.

“Mimi sijui chochote ndiyo mnaniambia, lakini kama Lulu amevishwa pete ya uchumba, basi ninamtakia kila la heri na mwanangu Kanumba apumzike kwa amani huko aliko. “Sina mengi ya kuzungumza, kuhusu hayo ya zamani nilishamwachia Mungu, siwezi kuyarudia kuyazungumza tena kwa sasa,” alisema mama Kanumba.

Comments

Popular posts from this blog