Prince William, Kukutana na Rais Magufuli

Mwanamfalme William wa Uingereza
Mwanamfalme  (Prince) William wa Uingereza anapangiwa kukutana na Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki ijayo wakati wa ziara yake ya siku saba Afrika. Anatarajiwa kuzuru pia Kenya na Namibia katika ziara hiyo ambayo si ya kikazi. Ziara hiyo itafanyika kuanzia 24 Septemba hadi 30 Septemba. Lengo kuu litakuwa kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama.
Atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust. Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili. Akiwa ziarani Tanzania, atafanya mashauriano na Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo katika kukabiliana na ujangili kwa mujibu wa shirika la habari la Press Association.
Kadhalika, atazuru bandari ya Dar es Salaam kujifahamisha zaidi kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo. Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama. Mwaka 2013, mwezi Oktoba, ilizindua Operation Tokomeza Ujangili ingawa ilisitishwa takriban mwezi mmoja baadaye, huku watetezi wa haki wakiwalaumu waliokuwa wanaendesha operesheni hiyo kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Tanzania ilikuwa na tembo 110,000 mwaka 2009 lakini idadi hiyo imeporomoka hadi kufikia tembo 43,000 kutokana na ujangili. Moja ya malengo ya ziara ya William ni kupigia debe mkutano mkuu wa kukabiliana na ujangili ambao utaandaliwa jijini London kati ya 11-12 Oktoba.
Mkutano huo ambao kwa kirefu unafahamika kama Illegal Wildlife Trade Conference, unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori, kwa kuangazia mambo matatu makuu: ulanguzi wa wanyama, wadudu na mimea kama uhalifu, kujenga ushirikiano na kufunga masoko yanayotumiwa na wahalifu kulangua wanyamapori.Image result for magufuli
Taarifa ya Kensington Palace inasema ingawa atakuwa katika ziara ya kibinafsi, ameombwa na Malkia kutekeleza shughuli kadha rasmi kwa niaba yake. Akiwa nchini Kenya, William atatembelea kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha 1st Battalion cha Irish Guards Battlegroup nchini Namibia, anatarajiwa pia kukutana na Makamu wa Rais, Nangolo Mbumba,  na pia atahudhuria hafla ya kusherehekea ushirikiano kati ya Uingereza na Namibia katika makazi ya balozi wa Uingereza nchini humo Kate Airey.
William ameeleza wazi upendo wake kwa bara Afrika.   Aliomba posa kutoka kwa mkewe Kate Middleton wakiwa katika mgahawa mmoja wa porini karibu na Mlima Kenya mwaka 2010.  William, 36, majuzi alipokuwa anakubali kuwa mlezi wa shirika la Royal African Society alieleza anavyolipenda bara hilo.
“Nilianza kuipenda Afrika mara ya kwanza nilipokaa kwa muda Kenya, Botswana na Tanzania nikiwa bado kijana mdogo. Nilifurahia sana na nimekuwa nikitaka kurudi mara kwa mara kadiri iwezekanavyo tangu wakati huo,” alisema
Mara ya mwisho kwake kuzuru Kenya ilikuwa mwaka 2016 ambapo alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na kushauriana kuhusu usalama na uhifadhi wa wanyama. Wengi watasubiri kuona iwapo atasafiri na Catherine ambaye  amekuwa katika likizo ya uzazi tangu mwezi Machi alipojifungua mwanaye Louis.
Anatarajiwa kurejelea majukumu yake rasmi karibuni. Wamejaliwa watoto wengine wawili, George, 5, na Charlotte, 3.     William ni wa pili katika orodha ya warithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza baada ya babake Prince Charles.

Comments

Popular posts from this blog