Mwanakwaya Aliyeuawa Gesti, Familia Yasimulia Mazito


DAR ES SALAAM: Tukio la mwanakwaya wa Kwaya ya Vijana ya Kanisa la AICT-Chang’ombe (CVC) Mariam Charles, 25, (pichani) mkazi wa Keko Furniture, wilayani Temeke jijini Dar aliyekutwa ameuawa kwenye Gesti ya East London, Mtaa wa Kwa Hamad Bonge, Temeke limeendelea kutikisa mjini na Risasi Jumamosi linakupa undani wake.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba 5, mwaka huu katika nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia mchumba wake aliyetajwa kwa jina la Frank ambaye amehusishwa na mauaji hayo.

TUMSIKILIZE KAKA WA MAREHEMU
Akizungumza kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Enock Charles, alisema kwamba alipata taarifa za kifo cha mdogo wake siku ya Jumatano (Septemba 5) asubuhi baada ya kutumiwa ujumbe na mama yao mzazi.
“Mimi ninaishi Kigamboni, Jumatano asubuhi nikiwa kwenye mishemishe zangu, mama alinitumia SMS kwamba kuna matatizo nyumbani.

“Nilimuuliza ni kuhusu nini akaniambia ni kumhusu Mariam. Nilishangaa kwa maana siku ya Ijumaa (jana) tulikuwa tuna taarifa kwamba angetolewa mahari na mchumba wake aitwaye Frank,” alieleza kaka huyo wa marehemu.

UJUMBE KUTOKA KWA FRANK
Enock aliendelea kusimulia kwamba, baada ya kufika nyumbani kwao alikuta hali ya vilio jambo lililomshangaza, baada ya kuuliza vizuri ndipo alipoelezwa kwamba ndugu yao Mariam alikutwa amefariki dunia gesti.

“Mbali na hilo kuna ujumbe ambao mama alikuwa ametumiwa kwenye simu yake kutoka kwenye namba ya mchumba wake Frank. Ujumbe huo ulisomeka kwamba; ‘Nimeamua kumuua Mariam kwa sababu ya uongo wake. Nimemfuma akizungumza uongo na mtu anayenidai akimpa taarifa kwamba nimerudi’.

“Baada ya kupata taarifa hizo ilibidi twende kutoa taarifa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi cha Keko, baadaye wapelelezi wa Kituo cha Polisi cha Temeke ndiyo walilichukua hili suala kwa ajili ya upelelezi zaidi,” alieleza Enock.

MCHUMBA WAKE AZUA SINTOFAHAMU
chanzo cha habari chetu kilichokuwa msibani kilisikia waombolezaji wakihusisha kifo cha Mariam na mchumba wake huku wengine wakishindwa kukubaliana moja kwa moja na madai hayo.
“Hili tukio kwa kweli limeniweka njia panda, namjua vizuri Mariam na huyu mchumba wake, walikuwa wanapendana sana, sasa haya madai kuwa kuna uwezekano kifo cha Mariam, Frank anahusika, hapo ndiyo napata shida.

“Lakini sasa, kama hahusiki, iweje simu yake ndiyo iwe imetuma huo ujumbe kwamba amemuua tena kwa sababu ambazo hazina mashiko kabisa? Yaani ngoja tu tuliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake,” alisema Jonathan Alphonce ambaye ni jirani wa marehemu.

Aidha mmoja wa wanakwaya ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema:
“Hapa si bure, itakuwa ni huyo huyo mchumba wake ndio kahusika. Haiwezekani amuite halafu mwenzake auawe halafu yeye tusimuone, amekwenda wapi?
“Kama hiyo haitoshi, simu yake hiyo hiyo ndio imetuma ujumbe wa kuonesha amefanya mauaji hayo. Mimi kwa kweli naona huyu mchumba wake kama yuko hai, atakuwa na siri nzito ya kifo hiki.”

DADA MTU ANENA
Dada wa marehemu, Pendo Charles ambaye alisema aliumizwa mno na kifo cha mdogo wake.
Akizungumzia kuhusu kuhusishwa kwa mchumba wa marehemu aitwaye Frank, alisema hivi;
“Siku ya Jumanne ndipo mchana ndipo marehemu alipoondoka nyumbani. Alimuaga mama kwamba angepitia kwenye biashara zake ndogondogo kisha baadaye angekwenda kanisani kwani alikuwa ni muimba kwaya kwenye Kanisa la AICT Chang’ombe.

“Basi akaondoka, lakini baada ya kufuatilia kwa kuwauliza wanakwaya wenzake walisema hakwenda kanisani siku hiyo. Lakini yeye mwenyewe majira ya jioni alimtumia SMS mama kwamba siku hiyo asingerudi nyumbani, bali angelala kwa mchumba wake Frank kwa ajili ya kupanga naye masuala yao ya utoaji mahari ambayo yalikuwa yafanyike Ijumaa (jana).

“Kwa kuwa Frank alikuwa anajulikana nyumbani na suala la mahari lilikuwa linafahamika, mama hakuona sababu ya kumzuia au kumfokea, alimruhusu akalala huko, lakini siku iliyofuata ndipo tulipopokea ujumbe wa kifo chake kutoka kwenye namba ya Frank,” alisema Pendo.

WOTE WALIKUWA WANAKWAYA!
Dada wa marehemu Pendo aliendelea kuweka wazi kwamba, marehemu Mariam na mchumba wake huyo Frank, wote walikuwa ni wanakwaya wa Kanisa la AICT Chang’ombe na walikuwa wakionesha kupendana sana.

BABA WA MAREHEMU NAYE…
Akizungumzia tukio hilo, baba wa marehemu Charles Lutonja, alisema limetokea siku ambayo mchumba wake alitoa taarifa za ghafla kwamba anataka kutoa mahari.
“Frank alishatoa posa Aprili mwaka huu lakini ghafla tu tulishangaa anasema anakuja Dar akitokea Dodoma kuja kutoa mahari.

“Nilishangaa lakini hata hivyo nilikubali, kweli alipofika akampigia simu mke wangu akamuomba binti yangu aende kukutana naye katika nyumba ya wageni aliyofikia. Mama yake alimruhusu na hatukumuona tena hadi tulipopewa taarifa za msiba, Jumatano,” alisema mzazi huyo.

Mzazi huyo alisema wameliacha jeshi la polisi lifanye kazi yake ya uchunguzi lakini wao wameruhusiwa kuzika na walitarajia kufanya hivyo leo (Jumamosi).
Hadi gazeti hili linaondoka msibani hapo, majibu ya uchunguzi wa polisi yalikuwa hayajatoka, lakini pia mtuhumiwa alikuwa hajapatikana kwani alikuwa hajulikani alipo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alikiri kuwa na taarifa za tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu.

KUZIKWA LEO
Mazishi ya mwanakwaya huyo yanatarajia kufanyika leo katika Makaburi ya Temeke jijini Dar.
Bwana Ametoa…..Bwana Ametwaa Jina lake lihimidiwe. Pumzika kwa Amani Mariam.

Comments

Popular posts from this blog