RAIS MAGUFULI APONGEZA JIMBO LA MBULU KUPATA ASKOFU MPYA
Waziri wa Katiba na Sheria profesa
Palamagamba Kabudi na Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti na
viongozi mbalimbali wakifuatilia misa Takatifu ya kumweka wakfu Askofu
wa Jimbo la Mbulu Anthony Lagwen.
Askofu wa Jimbo la Mbulu Anthony Lagwen akiwekwa wakfu kuwa askofu wa Jimbo hilo mjini Mbulu Mkoani Manyara jana.
Askofu wa Jimbo la Mbulu Anthony
Lagwen akiwa kwenye kiti chake baada ya kusimikwa kushika nafasi hiyo
mjini Mbulu Mkoani Manyara jana, kushoto ni Askofu Mkuu wa Jimbo kuu
katoliki la Dar es salaam mhadhama Polycap Kardinali Pengo na Askofu
mwandamizi Yuda Thadeus Ruwaichi.
Waziri wa Katiba na Sheria profesa
Palamagamba Kabudi akimkabidhi Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu
Anthony Lagwen, zawadi iliyotolewa na Rais John Pombe Joseph Magufuli
baada ya Askofu huyo kusimikwa jana mjini Mbulu Mkoani Manyara.
RAIS John Magufuli
amewapongeza wananchi wa wilaya za Mbulu, Babati na Hanang’ mkoani
Manyara na Karatu mkoani Arusha zinazounda Jimbo la Mbulu kwa kumpata
askofu wa tano wa Jimbo hilo Anthony Lagwen.
Waziri wa Katiba na
Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alimwakilisha Rais Magufuli
aliyasema hayo jana mjini Mbulu Mkoani Manyara, kwenye tukio la
kusimikwa kwa askofu Lagwen.
Waziri kabudi alisema
pamoja na kuwapongeza, kanisa katoliki limekuwa msaada mkubwa kwa
serikali kwa kutoa huduma ya elimu, afya na maji hasa kwa watu wa
kawaida.
Alisema jimbo la Mbulu
linaloundwa tangu mwaka 1953 limekuwa mfano wa kuigwa katika kuhakikisha
jamii ya eneo hilo inapata huduma za kiroho na kimwili.
“Tunapongeza kanisa
katoliki jimbo la Mbulu kwa kutoa huduma za afya ikiwemo hospitali za
misheni za Dareda na Bashnet wilayani Babati,” alisema.
Alipongeza jimbo hilo
kumiliki kituo cha redio Habari Njema ambacho kwa namna moja au nyingine
kinatoa huduma ya uinjilishaji na kuhabarisha jamii.
“Kituo hicho cha redio kiendelee kusisitiza amani kwani bila uwepo wa amani hakutawezekana kufanyika chochote,” alisema.
Alisema taasisi za dini
kwa kiasi kikubwa zimechangia maendeleo mengi na ustawi wa jamii hivyo
serikali itaendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha jamii
inasonga mbele.
Askofu mkuu wa Jimbo kuu
la Dar es salaam, mwadhama Policarp Kardinali Pengo alisema japokuwa
askofu Lagweni ni mzaliwa wa jimbo la Mbulu lakini atakumbana na
changamoto zile zile wanazokumbana nazo maaskofu ambao wanaongoza
majimbo ambayo hawajazaliwa.
“Mimi siwezi kuona
Sumbawanga ndiyo bora zaidi kuliko sehemu ninayoongoza waumini hivyo
nawe waongoze waamini kama inavyopaswa kuwaongoza,” alisema Kardinali
Pengo.
Rais wa baraza kuu la
maaskofu wakatoliki nchini (TEC) askofu wa jimbo la Mpanda, Gervas
Nyaisonga alisema askofu Lagwen ameteuliwa na Baba mtakatifu papa
Francisco wakati huu ambapo wanasherehekea jubilee ya miaka 150 ya
uinjilishaji.
Askofu Nyaisonga alisema
askofu Lagwen baada ya kupata nafasi hiyo anapaswa kuwaangalia usoni
waumini ili kuzidi kuwajenga kiroho.
Mkuu wa mkoa wa Manyara,
Alexander Mnyeti alisema serikali ya mkoa huo itashirikiana na jimbo
hilo katika kufanikisha ustawi wa wananchi wa eneo hilo.
Mnyeti alisema askofu
Lagweni amepata daraja hilo la uaskofu ambapo ni heshima kwa wananchi wa
Mbulu, Manyara na Tanzania kwa ujumla.
“Japokuwa wewe umezaliwa
katika jamii ya wairaqw hata ungekuwa mmeru au msukuma lakini kwa kuwa
umeteuliwa kuwa askofu wa Mbulu, umepakwa mafuta kwa uwezo wa roho
mtakatifu,” alisema Mnyeti.
Akizungumza baada ya
kusimikwa askofu Lagwen alisema anamuomba Mungu amsaidie kutimiza wajibu
wake mpya wa kiroho katika kuwahudumia waamini wa eneo hilo.
Askofu Lagwen alisema
wanashirikiana na serikali katika kufanikisha huduma mbalimbali na
miradi ya elimu, afya, maji, mazingira, habari na nyingine.
Aliwashukuru wote
walifanikisha tukio hilo na akawaahidi kuwa atatoa ushirikiano
unaostahili kupitia nafasi yake kwa upendo na umoja watumikie.
Askofu Anthony Lagwen
alizaliwa Julai 5 mwaka 1967 kwenye Kijiji cha Tlawi, wilayani Mbulu
mkoani Manyara na kuanza masomo ya elimu ya msingi na masomo ya
sekondari katika seminari ndogo ya Sanu, Jimbo Katoliki la Mbulu.
Comments
Post a Comment