KIFO CHA MAJUTO… KILICHOMTOA FAHAMU TAUSI CHA JULIKANA
SIRI ya muigizaji Tausi Mdegela, kuangua kilio kupita kiasi kwenye msiba wa nguli wa vichekesho Bongo, Amri Athuman ‘King Majuto’ wiki iliyopita imebainika kuwa msanii huyo alikuwa ni baba yake wa hiari aliyemfundisha sanaa ambayo sasa inamweka mjini.
Akizungumza na Ijumaa wa Wikienda, Tausi alisema kuwa, Majuto alikuwa baba yake aliyemlea katika maadili mema na aliyetamani sana kumuona anafika mbali kisanaa kwani ndio aliyemfundisha na alikaa naye nyumbani kwake Tanga kwa muda mrefu kama mwanaye wa kumzaa.
“Mimi hapa nalia kwa uchungu mkubwa naumia mno kumpoteza baba yangu aliyenilea katika kazi kwa sababu ni mtu ambaye alikuwa anataka kujua hali yangu kila mara na alipenda mno kuona maendeleo yangu kila siku kama mwanaye,” alisema Tausi.
Akiendelea kuzungumza na gazeti hili kwa uchungu, Tausi alisema kuwa Mzee Majuto hata wakati anakaribia kufariki yeye alikuwa ametoka nje kidogo ya Jiji la Dar lakini alipigiwa simu na dairekta Leah Mwendamseke ‘Lamata’ na kumueleza kwamba anaitwa na Majuto na kweli akawahi kumuona kabla hajakata roho.
“Kama baba angefariki bila mimi kumuona kwa kweli ningeumia sana sana lakini nakumbuka alimwambia dada Lamata, Tausi yuko wapi ndipo aliponipigia simu na kuniambia popote nilipo nirudi nije kumuona baba na kwa bahati mbaya baada ya kumuona pale hospitali kesho yake akafariki,” alisema Tausi huku machozi yakimtoka.
Msanii huyo aliendelea kusema kuwa pamoja na kumpoteza baba yake huyo wa hiari lakini anamshukuru Mungu amemtimizia ndoto yake na ameweza kumtengenezea jina ambalo mpaka sasa anapata kazi mbalimbali za kucheza filamu.
Comments
Post a Comment