JPM Apiga Marufuku Wamachinga Kunyanga’nya Bidhaa
Rais Dkt. John Magufuli amewapiga marufuku viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kuwanyang’anya bidhaa wafanyabiashara wadogo na badala yake amewaagiza viongozi wote nchini kujielekeza katika kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Agosti 18, 2018 alipokuwa anasalimiana na wananchi waliokusanyika mjini Sengerema akiwa njiani kuelekea Chato Mkoani Geita kwa mapumziko, ambapo wananchi hao walidai halmashauri ya Wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza matunda yao mjini hapo.
“Nilishasema viongozi wote niliowateua mimi msisherehekee uteuzi, mtasherehekea siku mkimaliza uongozi, nataka mchape kazi, tatueni kero za wananchi na waleteeni maendeleo”, amesema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.
Mbali na hilo, Dkt. Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.
“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu tunakwenda vizuri, juhudi zetu za kujenga Tanzania mpya zinapata mafanikio makubwa, tumejenga viwanda vingi, nataka tuirudishe Tanzania ya Nyerere ambapo hapa Mwanza kulikuwa na viwanda vingi na vijana wengi walipata ajira”, amesema Rais Magufuli.
Hii si mara ya kwanza Rais Dkt. John Magufuli kuwatetea wafanyabiashara wadogo wadogo, itakumbukwa mnamo Julai 16, 2018 aliwaruhusu wafanyabiashara wadogo wadogo wa eneo la Mbezi jijini Dar es Salaam kuendelea kufanya biashara zao pembezoni mwa barabara, huku akizitaka mamlaka husika zisiwanyanyase wafanyabiashara hao wanaotafuta riziki.
Comments
Post a Comment