WAZEE WA NITUMIE PESA KWA NAMBA HII’… WANASWA


IRINGA: Yawezekana wewe ni kati ya watu ambao walishawahi kutumiwa meseji za kitapeli kutoka kwa watu hao (pichani) ambao huandika hivi; ‘ile pesa nitumie kwenye namba hii, jina litatokea…, simu yangu ina tatizo’.

Kama jibu ni ndiyo basi habari ikufikie kwamba, watuhumiwa wengine wapatao saba wa utapeli huo hivi karibuni wamenaswa mkoani Iringa baada ya kuwaliza watu wengi kwa muda mrefu. Watu hao wamekuwa wakiwatumia watu meseji na kuwaelekeza kuwa watume pesa, mazingira ambayo baadhi huenda walikuwa na watu ambao ilikuwa wawatumie pesa hivyo hutuma na kujikuta wametuma kwa matapeli hao.

POLISI WATANGAZA VITA
Kufuatia kushamiri kwa utapeli huo katika mikoa mbalimbali, jeshi la polisi kupitia kwa makamanda wa mikoa hivi karibuni lilitangaza vita dhidi ya uhalifu huo na kufanikiwa kuwanasa baadhi ya watu huku tahadhari ikitolewa kwa wananchi kuwa makini wanapokumbana na meseji za aina hiyo.

WALIONASWA IRINGA
Mbali na wale 15 wa hivi karibuni waliokamatwa jijini Dar, wengine saba juzikati walinaswa na polisi mkoani Iringa wakiwa kwenye mishemishe ya kuwaliza watu. Watu hao walikamatwa wakiwa na simu 19, madini feki ya dhahabu, maburungutu ya pesa feki na hirizi tatu, moja ikidaiwa ilikuwa ‘ikipumua’. Akiwazungumzia watuhumiwa hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema waliwakamata nyakati tofauti kufuatia mtego uliokuwa umewekwa na vijana wake.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na kiongozi wao Emmanuel Tweve (41) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Tabata, Dar ambaye baada ya kukamatwa na kufanyiwa upekuzi kwenye gari lake aina ya Toyota Brevis lenye namba za usajili T 419 ALL, alikutwa na noti bandia 63 mfano wa Dola za Kimarekani na madini bandia ya dhahabu Kg 3.5

Pamoja na kiongozi huyo pia jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata wahusika wa mtandao huo ambao ni Abdallah Mohammed (43) mkazi wa Madoto Mburahati, Abubakar Mohammed (40) mkazi wa Mbarali- Mbeya, Seif Seleman (37) mkazi wa Chanika, Christopher Mgia (37) Mkazi wa Itamba -Makete, Frank Lutalile (54) Mkazi wa Mbeya na Ahabu Mbina mkazi wa Mbarali, Mbeya.

Emmanuel Tweve (kiongozi wa kundi) baada ya kubanwa na polisi alikiri kwamba wamekuwa wakipata fedha nyingi kwa utapeli huo na kuomba wananchi wasikubali kuendelea kutapeliwa. Kamanda Bwire aliwataka wananchi mkoani Iringa na kwingineko nchini kuwa makini na utapeli huo kwa kuepuka mawasiliano na watu wasioeleweka.

Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi mkoani Iringa limefanikiwa kuwakamata watu wawili waliodaiwa kuhusika kwenye tukio la ujambazi lililotokea hivi karibuni katika eneo la Wililesi, Kata ya Gangilonga nyumbani kwa mfanyabiashara Faraj Abri.

Kamanda Bwire alisema Juni 13, mwaka huu majambazi hao zaidi ya sita waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya mfanyabiashara huyo kwa lengo la kupora lakini waligonga mwamba. “Baada ya kuingia ndani walifyatua risasi mbili za bastola ambazo zilimjeruhi mtoto wa mfanyabiashara huyo katika paja la mguu wa kushoto hali iliyosababisha familia ya mhanga huyo kupiga simu kwa jamaa zao ambao walifika na kuanza majibizano ya risasi na majambazi hao ambao baadaye walikimbia,” alisema Kamanda Bwire.

Alisema baada ya msako mkali walifanikiwa kuwatia nguvuni watu wawili wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo na msako zaidi unaendelea ili kuwanasa wengi waliohusika na sheria ichukue mkondo wake.
Stori: Francis Godwin, Amani.

Comments

Popular posts from this blog