TAGCO NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZAPONGEZWA KWA UTENDAJI
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Tunduru Bw. Chiza Marando akisisitiza kuhusu namna Halmashuri
hiyo ilivyojipanga katika kuimarisha mawasiliano ya kikakati hasa
kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Tunduru Bw. Chiza Marando akisisitiza jambo kwa ujumbe wa
chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya
Habari MAELEZO wakati wa ziara ya ujumbe huo katika Halmashauri hiyo
kukagua na kujionea jinsi maafisa Habari wanavyotekeleza jukumu la
kuisemea Serikali katika Mikoa na Halmashuri zao.
Kiongozi wa Ujumbe wa Viongozi wa
Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) na Idara ya
Habari (MAELEZO) Bi. Gaudensia Simwanza akisisitiza jambo kwa Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Bw. Chiza Marando wakati
wa ziara ya ujumbe huo katika Halmashuri hiyo uliolenga kukagua na
kuweka mikakati ya pamoja katika kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa
umma.
Mwakilishi wa Idara ya Habari
MAELEZO Bw. Casmir Ndambalilo akisisitiza umuhimu wa Maafisa Habari na
Mawasiliano Serikalini kuwajibika katika kuisemea Serikali hasa
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa na Halmashuri zao, hiyo
ilikuwa katika ziara iliyoandaliwa na Chama cha Maafisa Habari na
Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Idara ya Habari
MAELEZO.
Frank Mvungi- MAELEZO, Tunduru
Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano
Serikalini (TAGCO) na Idara ya Habari (MAELEZO) vimepongezwa kwa kubuni
na kuweka utaratibu wa kufuatilia utendaji wa Maafisa Habari na
Mawasiliano Serikalini hadi katika ngazi ya Halmashuri.
Akizungumza na Ujumbe wa chama hicho
uliofika Ofisini kwake mapema wiki , Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya hiyo Bw. Chiza Marando amesema kuwa hili ni jambo la kihistoria
ambapo ufuatiliaji wa utendaji wa Maafisa Habari unafanyika katika
ngazi zote.
“Tangu nimeanza kazi sijawahi kushuhudia
ufuatiliaji wa namna hii na sisi tuko tayari wakati wote kutoa
ushirikiano utakaosaidia Afisa Habari katika Halmashauri yetu atekeleze
majukumu yake vizuri hasa katika kutangaza miradi ya maendeleo”
Alisisitiza Marando
Akifafanua Bw. Marando amesema kuwa
Halmashuri yake inatambua umuhimu wa mawasiliano kati ya Serikali na
Wananchi hivyo imeweka kipaumbele katika kuwezesha utoaji wa taarifa za
maendeleo kwenda kwa wananchi ili waweze kushiriki katika kujiletea
maendeleo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Msafara wa
Viongozi wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO)
na Idara ya Habari – MAELEZO Bi. Gaudensia Simwanza amesema kuwa
maafisa habari wanalo jukumu kubwa katika Halmashauri na Mikoa katika
kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo
yao.
Aliongeza kuwa kutokana na jukumu hilo wanapaswa kutumia rasilimali zilizopo kutekeleza jukumu hilo kwa weledi.
Ziara ya Viongozi wa Chama cha Maafisa
Habari na Mawasiliano Serikalini na Idara ya Habari MAELEZO inafanyika
katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa
kufuatilia na kuona utendaji wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini
katika ngazi zote ili kutoa msukumo na kuweka mikakati ya pamoja katika
kuimarisha Mawasiliano ya Serikali kwa umma ili kuchochea maendeleo na
ustawi wa wananchi.
Comments
Post a Comment