Simba Kufikia Kambi ya Kishua Uturuki

JUMLA ya wachezaji 26 wa kikosi cha Simba, wanatarajiwa kuondoka kesho Alfajiri kuelekea Uturuki kuweka kambi ya takribani wiki mbili kabla ya kurejea hapa nchini Agosti 5, mwaka huu.
Wachezaji wa Simba ambao watakuwa kwenye safari hiyo jana Ijumaa walikuwa na zoezi la upimwaji wa afya kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar. Katika nyota hao 26 watakaosafiri, kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto, hatakuwepo kwenye msafara huo ambao utaongozwa na kocha mpya wa kikosi hicho, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji. Msafara mzima wa Simba unaotarajiwa kwenda Uturuki kwenye kambi hiyo, utakuwa na jumla ya watu 35.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kimelidokeza Championi kuwa, mbali na Kazimoto, pia Mosses Kitandu, Jamal Mwambeleko, Ally Shomary na Said Mohammed ‘Nduda’ nao watabaki hapa nchini.

“Kama ambavyo imepangwa, kikosi kitaondoka Jumapili alfajiri ambapo baada ya kocha mpya kutangazwa jana (juzi Alhamisi), yeye ndiye atakuwa anawaongoza vijana wake hao sambamba na msaidizi wake, Masoud Djuma.
“Lakini kabla ya kikosi hakijaondoka, kocha atatambulishwa mbele ya wachezaji wote,” kilisema chanzo hicho.

KUFIKIA KAMBI YA KISHUA
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Umoja wa Utalii wa Michezo wa Uturuki, Samil Yasacan sehemu inapokwenda kuweka kambi Simba wikiendi hii mwaka jana zilifurika timu za soka 1500 kutoka dunia nzima.

Antalya ni mji maarufu wa kitalii ulioko umbali wa saa moja na dakika 15 kwa ndege kutoka mji mkuu wa Uturuki, Istanbul. Umbali kutoka Dar es Salaam mpaka Istanbul ni kilomita 5420 kwa ndege sawa na saa 7. Ambako huko kunasifika kwa kuwa na hoteli zenye hadhi ya juu ‘kishua’ na Simba itafikia kwenye moja kati ya hoteli hizo.

KUCHEZA MECHI TATU ZA KIRAFIKI
Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma ameliambia Championi Jumamosi kuwa, kwa wiki mbili watakazokuwa kwenye mji huo wenye viwanja vingi vya kisasa vya michezo wamepanga kucheza mechi tatu za kirafiki ambapo wiki ya kwanza baada ya kufika watafanya mazoezi na ile ya pili ndiyo watajipima.

“Hatutacheza mechi nyingi ni mbili au tatu inategemea na siku ambazo tutakaa. Kwa upande wa Salamba yeye bado anaumwa kwa hiyo anaendelea na matibabu na kule tunaenda kufanya mazoezi hatupeleki mgonjwa,” alisema Djuma ambaye anakubalika na mashabiki wa Simba.

Comments

Popular posts from this blog