Nyumba mbili zachomwa Moto Mwanza kisa wizi

Na Paschal D.Lucas, Mwanza
Wananchi waliojichukulia sheria mkono wamechoma nyumba mbili za familia moja na nyingine kuziharibu katika mtaa wa Nyakabungo "A" kata ya Isamilo wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza  baada ya kuona watoto wa familia zile wanajihusisha na uhalifu hapo mtaani hapo mara kwa mara.

Maamuzi hayo yamekuja baada ya wananchi kudai kuwa watoto hao wamekuwa wakikamatwa na kupelekwa mahakamani kushitakiwa lakini mara nyingi wamekuwa wakiachiwa kwa dhamana na kurudi mtaani kuendelea tena na tabia hiyo kitendo ambacho kimekuwa ni kero kubwa  kwa wananchi wa eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 usiku wa tarehe 25,Julai 2018 ambapo katika tukio hilo nyumba mbili zilizoharibiwa ni mali ya Selina Francis (50) na Abdallah Mwita wote wakiwa ni wakazi wa Nyakabungo mkoani humo.

Vile vile nyumba moja mali ya Manka Francis James iliharibiwa vibaya na kundi hilo kwa kuvunjwa milango na madirisha na kuharibu vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani kwa kumtuhumu mwanamke huyo kuwa  anashirikiana katika kuwaficha wezi na vibaka ikiwa ni pamoja na kujihusisha na utapeli kwa wananchi wa mtaa huo  kwa kuwauzia dhahabu bandia kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Inadaiwa kuwa wananchi wa mtaa huo wamekuwa wakimlalamikia na kumtuhumu mtoto wa wa Mama Selina Francis aitwaye Mkapa Mwabe pamoja na mtoto wa mzee Abdallah  Mwita aitwaye Emmanuel Mwita kuwa ni wezi na vibaka mtaani hapo.

Inasemekana kutokana na tuhuma hizo wananchi waliojawa na hasira kutokana na vitendo hivyo walikwenda na kuvamia na kukuta watoto wadogo na wenye nyumba hawakuwepo kisha kuwatoa watoto nje na kuchoma nyumba hizo moto.Aidha inadaiwa kuwa baada ya kuchoma nyumba hizo walihamia kwenye nyumba ya Mama Selina Francis napo walikuta watoto wadogo na wenye nyumba hawakuwepo hivyo wakavunja na kuharibu vitu vilivyokuwemo.

Baada ya kitendo hicho raia wema walitoa taarifa kwa polisi ambapo askari waliokuwa doria walifika haraka eneo hilo na kukuta tayari wahalifu hao wameshaondoka.Msako mkali wa kuwatafuta wale wote waliohusika na namna moja au nyingine  unaendelea  ikiwemo ufutiliaje wa kuwapata vijana wanaotuhumiwa kufanya uhalifu mtaani hapo  pamoja na wazazi wao.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu Kamishna wa polisi Ahmed Msangi ametoa onyo kwa watu wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria, na wale wote waliohusika endapo watabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Sambamba na hilo pia amewataka wananchi watambue kwamba dhamana ni haki ya mtuhumiwa endapo tu kama kesi anayotuhumiwa nayo inadhaminika hivyo wananchi waache tabia hiyo kwani pindi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana  ni hitaji kisheria wakati shauri linaendelea mahakani.

Aidha Kamanda Msangi anawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema za wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria

Comments

Popular posts from this blog