BETHIDEI YA TIFFAH KUFURU


DAR ES SALAAM: Maandalizi ya pati ya kuzaliwa (birthday) ya bintiye ambaye ndiye uzao wake wa kwanza, Latifah Nasibu ‘Tiffah Dangote’ (3), yamemfanya baba’ke ambaye ni staa wa muziki wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutoa kiapo kizito kuwa itakuwa ni shughuli ya kufuru, Risasi Jumamosi linakupa exclussive.
Agosti 6, mwaka huu, Tiffah atatimiza umri wa miaka mitatu tangu alipozaliwa Agosti 6, 2015, lakini sherehe hiyo imesogezwa mbele ambapo sasa itafanyika Agosti 17 hadi Agosti 20, mwaka huu.

DIAMOND NA RISASI JUMAMOSI
Akizungumza na Risasi Jumamosi juu ya pati hiyo ya Tiffah ya kutimiza umri wa miaka mitatu, Diamond alisema kuwa, yupo tayari kufilisika, lakini ahakikishe mwanaye huyo ana furaha kwa kumfanyia pati hiyo ambayo itakuwa ya kihistoria. “Nimepanga iwe sherehe kubwa sana, acha nifilisike, lakini mwanangu afurahi,” ndivyo alivyoanza Diamond kwenye mahojiano hayo maalum na Risasi Jumamosi na kuongeza:
“Nipo tayari kutumia sehemu ya pesa zangu za ziara yangu ya Marekani kwa ajili ya kuhakikisha mwanangu anakuwa na furaha. Kila kitu cha maandalizi kinakwenda sawia kabisa.”
SABABU YA KUSOGEZWA
Diamond aliendelea kufunguka kwamba, sababu hasa ya kusogeza sherehe hiyo kutoka Agosti 6, mwaka huu hadi Agosti 17 ni kutokana na ratiba yake ya kikazi kubana ambapo kwa sasa anaendelea na ziara ya shoo kwenye miji mbalimbali nchini Marekani.

“Sherehe itachukua wikiendi nzima, lakini ukijumlisha na maandalizi ya kuhakikisha wageni wamefika, itachukua wiki nzima. Siyo tukio la kitoto, nitahakikisha inakuwa ni shughuli ya kiwango cha juu. “Kama nilivyosema awali, nimetoa ofa kwa watoto 10 na wazazi wao (baba na mama hivyo jumla ni 30) ambao nao watasafiri kwenda South (Sauz) kutoka Bongo kwa ajili ya kusherehekea na Tiffah.

“Katika kuhakikisha watu wangu hao 30 watakaopata ofa ya kwenda Sauz wanasafiri salama kwa ndege mbili ambazo tutakodi kutoka hapa Bongo, wanakula na wanalala sehemu nzuri kwa siku zote, Kampuni ya GSM ndiyo itayosimamia upande mzima wa safari. Yaani kuanzia ndege na hoteli kwa siku zote watu wangu hao 30 watakazokaa huko Sauz hadi kurudi Bongo.
KURUSHWA LIVE
“Pia nimeeleza kuwa, kwa wasiobahatika kwenda Sauz, wasisahau kufuatilia shughuli nzima maana itarusha ‘live’ kupitia WasafiTV,” alisema Diamond ambaye mbali na Tiffah, pia amezaa na Zari mtoto wa kiume aitwaye Nillan.
MASTAA WA KUMWAGA
Diamond alipoulizwa juu ya kuwepo kwa mastaa wakubwa wa muziki duniani kwenye shughuli hiyo, alifunguka: “Siwezi kukutajia majina, lakini elewa tu kuwa watahudhuria wengi sana, mastaa watakuwa ni wa kumwaga kutoka sehemu mbalimbali Afrika. “Itakuwa ni shughuli ya kukata na shoka na kwa uhakika tu ni kwamba sijawahi kufanya shughuli kubwa kama hiyo.”
KWA NINI SAUZ?
Alipobanwa kwamba, kwa nini shughuli hiyo ifanyike Sauz na siyo Bongo, Diamond alisema: “Ndiko familia ilipo na ni jambo la uamuzi tu.” Risasi Jumamosi: Vipi kuhusu gharama? Je, umepanga kutumia shilingi ngapi? Diamond: Siwezi kukutajia kiasi, lakini ujue tu ni parefu. Lakini pia mambo mengine yanafanywa kwa udhamini wa makampuni.
ZARI AMFANYIA BONGE LA SHOPPING
Kwa upande wake, mzazi mwenza wa Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ amekuwa akiposti vipande vya video kwenye SnapChat akimfanyia Tiffah bonge la shopping ikiwemo kumnunulia vidani vya dhahabu.
NINI KINAENDELEA?
Diamond na Zari walitengana miezi kadhaa iliyopita, lakini wamekuwa wakiendelea kuwalea watoto wao, Tiffah na Nillan kwa pamoja ambapo watoto hao wanaishi na mama yao huyo huko Pretoria nchini Afrika Kusini.
source:GPL

Comments

Popular posts from this blog