Beki Simba atua Singida United kwa mkopo


Klabu ya soka ya Singida United imethibitisha kuwa imemsajili mchezaji Jamaly Mwambeleko kutoka Simba kwa usajili kamili tofauti na taarifa zilizoeleza kuwa wamemchukua kwa mkopo, huku wakiweka wazi kuwa wamemwongeza mwaka mmoja na sasa ni mchezaji wao kwa miaka miwili.

Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga ameeleza kuwa walifanya mazungumzo na Simba na kumalizana nao kisha kumpa mkataba wa mwaka mmoja Jamaly Mwambeleko lakini baadae walimwongeza mwaka mmoja na kuwa miwili.

''Tumemsajili Mwambeleko kwa usajili kamili wala hajaja kwetu kwa mkopo, ila awali mazungumzo yalikuwa hivyo lakini kocha Hemed Morocco akapendekeza tuwe naye kwa muda mrefu ndio akasaini mkataba wa kuitumikia Singida United kwa miaka miwili'', - amesema.

Jamaly Mwambeleko ambaye anacheza nafasi ya mlinzi wa kushoto ni sehemu ya wachezaji walioachwa na Simba katika usajili huu kwa kile kilichoelezwa ni kutokuwa na nafasi ya kucheza hususani nafasi yake pale Simba kuwa na wachezaji wenye viwango vikubwa ambao ni Asante Kwasi na Mohamed Hussein.

Singida United pia imekamilisha usajili wa kiungo Awesu Ally Awesu kutoka Mwadui Fc kwa mkataba wa miaka miwili. Tayari baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wapo kambini jijini Mwanza wakiendelea na maandalizi ya ligi kuu msimu ujao wa 2018/19.

Comments

Popular posts from this blog