Zitto amsifu Peneza kubadili taswira ya bajeti

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amempongeza Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Kigoma Upendo Peneza (CHADEMA) kuwa amefanikiwa kuacha alama ndani ya bunge la Tanzania akiwa na muda mfupi ndani ya bunge.

Zitto ametoa pongezi hizo ambapo amesema Peneza anaingia katika rekodi za Wabunge waliotumia nafasi yao kushawishi jambo lenye faida kubwa kwa jamii na likafanikiwa ikiwa ni baada ya Serikali kutangaza kuondoa kodi ya VAT kwenye Taulo za Kike zinazotumika na Wanawake kipindi cha hedhi.

“Kumekuwa na juhudi za kuleta mabadiliko haya miaka mingi kutokana na kazi za Mashirika kama TGNP Mtandao, SNV, Msichana Initiative nk. Upendo, licha ya kuwa na miaka 2 tu Bungeni aliweza kubeba hoja hii na kuiingiza Bungeni na kuunganisha Wabunge wote kutoka Vyama vyote.” ameandika Zitto

Ameongeza “Licha ya kwamba kampeni yake ilikuwa ni Watoto wa shule wapewe Taulo hizi bure ( litafika tu hilo kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa ), amepata mafanikio makubwa kwa uamuzi wa Serikali kuondoa VAT na hivyo kushusha gharama za Taulo hizi. Upendo ameacha alama ( legacy).” Zitto Kabwe

Amesisitiza “Mzee William Shelukindo aliwahi kunieleza tofauti ya kuwa Mbunge ( Member of Parliament ) na Mwana Bunge ( a parliamentarian). Kwamba Mwana Bunge ni Mbunge ambaye anaacha alama Katika kazi zake za Bunge na kwamba anaweza kuunganisha wabunge bila kujali Itikadi za Vyama Katika Hoja zenye maslahi ya Umma.”

Zitto amesema kuwa Peneza sasa amepanda daraja kutoka kuwa Mbunge na kuwa Mwana Bunge, a Parliamentarian huku akisisitiza kwamba ameipa Bajeti ya mwaka 2018/19 taswira ya BAJETI YA KIJINSIA”

Kituo cha East Africa Television LTD kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini imekuwa ikiendesha kampeni inayokwenda kwa jina la NAMTHAMINI kwa miaka miwili mfululizo imekuwa ikitoa msaada  wa taulo za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji kwa mwaka mzima.

Comments

Popular posts from this blog