Mkataba TanzaniteOne kufumuliwa

WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki, amesema serikali imeagiza leseni ya uchimbaji wa ubia baina ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML) ili utaratibu mpya uandaliwe kwa manufaa ya pande zote mbili.

Aliyasema hayo bungeni jana alipowasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kasoro iliyoibuliwa na Kamati Maalum ya Spika Kuchunguza Uchimbaji na Biashara ya Tanzanite katikati ya mwaka jana.

“Serikali imeagiza leseni ya uchimbaji wa ubia baina ya Stamico na TML irudishwe serikalini ili utaratibu mpya uandaliwe utakaoiwezesha serikali, TML na mwekezaji wa kimkakati kushirikiana katika uchimbaji, uendeshaji katika mgodi huo kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Madini, Sura ya 123 kama ilivyorekebishwa na Bunge mwaka 2017,” alisema.

Alibainisha kuwa mgodi wa ubia kati ya Stamico na TML ni miongoni mwa migodi ya tanzanite iliyopo Mirerani mkoani Manyara, akieleza kuwa ipo mingine inayomilikiwa na wachimbaji wazawa wenye leseni za uchimbaji mdogo na wa kati.

Alisema uendeshaji wa mgodi baina ya TML na Stamico umekuwa na changamoto nyingi zinazosababishwa na kasoro katika mkataba wa ubia na mkataba wa uendeshaji.

Alisema kutokana na kasoro zilizobainishwa na Kamati Maalum iliyoundwa na Spika, serikali iliagiza timu yake ya majadiliano kukutana na Stamico na wamiliki wa TML kujadiliana ili kubaini kasoro hizo na kupendekeza namna bora ya uchimbaji, biashara na uendeshaji wa mgodi kwa lengo la kunufaisha taifa kuliko ilivyo sasa.

Kairuki alisema kukamilika kwa majadiliano hayo ndiko kulikoifanya serikali iagize leseni ya uchimbaji irudishwe serikalini ili utaratibu mpya uandaliwe.

“Majadiliano na wachimbaji wadogo yanaendelea baina ya timu ya majadiliano ya serikali na wamiliki wa migodi hiyo kwa lengo la kuleta manufaa zaidi kwa taifa kutokana na madini ya tanzanite,” alisema Kairuki.

Waziri huyo alisema kuwa kwa kutambua umuhimu na upekee wa madini ya tanzanite duniani kwamba yanapatikana Tanzania tu, serikali inakamilisha utaratibu wa kuyatangaza madini hayo kuwa madini maalum.

Alisema utaratibu wa kuyatangaza utakamilika katika mwaka huu wa fedha uliobakisha siku 29 kufika ukomo.

Vilevile, waziri huyo alisema serikali kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha, itaendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu zinazotolewa katika Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (Teiti).

Alisema kuwa katika kipindi hicho pia wataanzisha rejista ya taarifa na majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.

Ili kutekeleza majukumu yake, Kairuki aliliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 58.908 kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Kati yake, Sh. bilioni 19.62 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Sh. bilioni 39.288 ni za matumizi ya kawaida.

Comments

Popular posts from this blog