TAJIRI AKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA, BASTOLA – DAR
MAMLAKA ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewatia mbaroni watuhumiwa wa biashara ya madawa ya kulevya, Ayoub Kiboko na mkewe, Pilli Kiboko, Mei 23, saa 8 usiku wakiwa nyumbani kwao eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam baada ya kuwasaka kwa muda mrefu.
Kiboko ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara waliotajwa katika barua za Watanzania waliofungwa Hong Kong, ni maarufu ndani na nje ya nchi na anadaiwa kumiliki hoteli kubwa zaidi ya 10 pamoja nyumba za kifahari katika maeneo mbalimbali hapa jijini.
Barua hizo zililetwa nchini Desemba 2014 na Kasisi John Wotherspoon anayesaidia wafungwa katika magereza ya Hong Kong na China na baada ya Watanzania hao kuandika barua hizo wakiwaasa wengine wasifanye biashara hiyo huku wakiwataja wafanyabiashara waliowabebesha dawa hizo za kulevya akiwamo Kiboko.
Kamishna wa Operesheni DCEA, Frederick Milanzi alisema katika msako uliofanywa nyumbani kwake usiku wa manane, walimkamata Kiboko akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin, gramu 250.
“Baada ya kumtia mbaroni akiwa na dawa hizo, tumetumia vifaa vyetu kupima dawa hizo na tukabaini ni heroin, lakini anayestahili kutoa majibu ni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hivyo tumeshapeleka sampuli kwa ajili ya uthibitisho na tunasubiri ikithibitika ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani mara moja,” alisema Milanzi.
Milanzi alisema walipofika katika jumba la kifahari la ghorofa mbili la mtuhumiwa huyo huko Tegeta, waliomba kumkagua lakini alikataa, maofisa walitumia mbinu zao na kufanikiwa kumkagua kisha kukamatwa dawa hizo pamoja na bastola ya kichina.
“Tulibaini ile bastola anaimiliki kihalali. Tulimkuta na unga mwingine ambao hatuwezi kutaja ni kiasi gani au ni wa aina gani mpaka utakapopimwa na mkemia mkuu wa Serikali, tumekamata baadhi ya mali zake yakiwamo magari yake matatu,” alisema Milanzi.
Inadaiwa mtuhumiwa huyo alianza biashara hiyo miaka mingi iliyopita na taarifa zinaonyesha kwamba huwatumia vijana mbalimbali kupeleka China baadhi yao wakiwemo walihukumiwa.
Aidha, Mei 23, Mamlaka hiyo imemtia mbaronui Abdul Omari Salehe (38), mkazi wa Mbezi kwa Msuguri katika eneo la kusafiria abiria Bandari ya Dar akiwa na pipi 10 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 150 alizokuwa akizisafirisha kwenda Zanzibar.
Milanzi alisema mtuhumiwa huyo aliachiwa huru hivi karibuni akitokea gerezani Hong Kong alikokuwa akitumikia kifungo cha miaka 10 na kwamba alitumwa na Salehe Ally Issa, mkazi wa Mbezi. Pia alikutwa na hati mpya ya kusafiria ya kielektroniki ambayo mtuhumiwa alidai ametengenezewa na Issa ili imsaidie kusafirisha dawa nchi mbalimbali. Hata hivyo, Issa naye alikamatwa Mei 24, akiwa nyumbani kwake.
Comments
Post a Comment