SHIDA YA UMEME KUSINI IMEKWISHA – MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema shida ya umeme iliyokuwa inaikabili mikoa ya Lindi na Mtwara hivi sasa imekwisha.
“Kuunganishwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara
kwenye gridi ya Taifa, kumeondoa tatizo la umeme lililokuwa likiikabili
mikoa hii, na mitambo ya jenerata iliyokuwepo, itabakia kuwa ya akiba
endapo dharura yoyote itatokea,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei
21, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Mtwara kwenye viwanja
vya bandarini mjini humo.
Alisema pengo lililokuwepo la
kukatikakatika kwa umeme, limezibwa kwa kupata umeme wa kutoka Somanga
hadi Lindi. “Umeme huu umeanzia kituo chetu cha Mbagala, umekuja
Mkuranga, Muhoro, Lindi na hatimaye umefika pale Mahumbika. Na mchana
wakati nikiwa Mahumbika, niliwasha kwa kompyuta kuashiria umeme wa gridi
kuingia mikoa yetu ya Lindi na Mtwara,” alisema.
Akiwa Mtwara mjini, Waziri Mkuu alikagua na
kisha kuzindua mradi wa upanuzi wa kituo cha kufua umeme wa gesi asilia
wenye uwezo wa kuzalisha megawati nne.
Kabla ya kuzindua mradi huo, alipita
bandarini kukagua ukarabati wa mitambo ya kupokelea mafuta ya dizeli na
petroli ambako alielezwa kuwa kampuni mbili za GM na OILCOM zimeanza
ukarabati na kwamba mwezi ujao, bandari hiyo itaanza kupokea meli za
kubeba mafuta.
“Bandari ya Mtwara hivi sasa itaanza
kupokea meli kubwa za mafuta, jambo ambalo halijafanyika tangu mwaka
2014. Mwezi ujao, wakati wowote, wataanza kupakua mafuta. Kwa hiyo mji
utaanza kuchangamka.”
“Kuanza kupakuliwa kwa mafuta katika
bandari hii, kutasaidia kushusha bei ya mafuta kwenye mikoa hii na pia
kiasi kitakachobakia, tutakipeleka nchi za jirani za Msumbiji na
Malawi,” alisema.
Alisema matengenezo hayo yakikamilika
yatafanya bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zote ziwe na uwezo
wa kupokea mafuta. Pia aliitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) iondoe urasimu
na Mkurugenzi Mkuu wake awatumie vizuri watendaji waliopo chini yake.
Mapema, walipopewa nafasi
ya kusalimia wananchi, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) walitumia
fursa hiyo kuelezea kufurahishwa kwao na hatua za maendeleo zinazofanywa
na Serikali ya awamu ya tano.
Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) aliwataka
wananchi wa mikoa ya Kusini wachangamkie fursa zinazopatikana kutokana
na maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano. “Kusini hivi
sasa imeamka na imetoka gizani, sasa wananchi tuchangamkie fursa,”
alisema.
Naye Mbunge wa Nachingwea,
Bw. Hassan Elias Masala, alitumia fursa hiyo kuomba barabara ya kutoka
Nachingwea iwekewe lami ili wakazi wake waweze kutumia fursa ya
kusafirisha korosho zao hadi kwenye bandari ya Mtwara.
Naye Bw. Maftaha Abdallah Nachuma (Mtwara
Mjini) pia aliomba barabara ya kutoka Mtwara hadi Mingoyo ikamilishwe
matengenezo yake kwani kwa hali ya sasa siyo rahisi kusafirisha mizigo.
Pia aliomba apelekewe umeme maeneo ya Mbawalachini na Mkunjanguo.
“Maendeleo hayana chama, kabila wala itikadi,” alisema.
Wabunge wengine waliofuatana na Waziri Mkuu
kwenye ziara hiyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bibi Hawa Ghasia na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini, Bi. Hamida Mohammed Abdallah (Viti Maalum).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 22, 2018.
Comments
Post a Comment