Mkutano Mkuu wa CCM Mambo Moto



MASIKIO ya wengi yameelekezwa kwenye mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika leo (Jumatatu) na kesho jijini Dar es Salaam, ambapo vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC ) vikitarajiwa kuwasha moto wa uamuzi mgumu unaotajwa kuwa ni nadra kutokea ndani ya chama hicho tawala.

Tangu mkutano huo utangazwe ukifuatiwa na kutolewa kwa ripoti ya ya uchunguzi wa mali za CCM nchi nzima kumekuwepo na habari nyingi zinazohusisha uwezekano wa vikao hivyo kutoka na maazimio mazito, hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya chama hicho kimeliambia Ijumaa Wikienda kuwa, agenda zake zitaleta mwangwi miongoni mwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

“Ni vikao vizito vitakavyoamua mambo mazito yenye faida kwa chama chetu, siwezi kusema ni yepi lakini tega masikio utasikia, CCM ni chama kikongwe na makini lazima mikutano yake hasa ya kitaifa iamue mambo makini .“Huwezi kuwa na chama kama hiki, kinachoshika dola halafu kiwe na mikutano ya kitotokitoto, wanaosema kitakuwa moto ni kweli kitakuwa moto hasa wala siyo uongo,” chanzo chetu kilichoomba hifadhi ya jina kwa sababu hakina mamlaka ya utoaji habari kilisema.
 
Ijumaa Wikienda lilishindwa kumpata Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikani na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ili walau atolee ufafanuzi uwepo wa madai kuwa chama hicho kupitia mkutano huo wa siku mbili utawang’oa katika nafasi zao baadhi ya makada wa chama hicho kutokana na kutuhumiwa kufuja mali za chama.

Jingine ambalo limekuwa likisemwa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii ni kufanyika kwa madadiliko ya uongozi kwa baadhi ya nafasi ambapo nafasi ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana inatajwatajwa kuwekwa mtu mwingine atakayeshika nafasi hiyo.
Takribani miaka mitatu tangu Rais John Pombe Magufuli achaguliwe kuwa rais na baadaye kupewa nafasi ya uenyekiti wa CCM kiongozi huyo aliahidi kufanya mageuzi ndani ya chama na serikali yenye lengo la kuleta tija katika taifa.

Katika kile kinachoonekana kuwa Rais Magufuli anaziishi kauli zake ameonekana kufanya mageuzi ya kuongoza Serikali kwa kupiga vita uzembe, ubadhilifu wa mali ya umma, ufisadi, watumishi hewa na kupambana na dawa za kulevya, wengi wanamtazama kuweza kufanya mageuzi ya aina hiyo ndani ya chama chake.

Hivi karibuni mwenyekiti huyo wa chama tawala aliunda tume iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Bashiru Ally Kakurwa, kufanya uchunguzi wa mali za chama ambapo Mei 21 mwaka huu tume hiyo ilimkabidhi ripoti ambayo rais huyo aliahidi kuifanyia kazi.
Licha ya kwamba CCM haijaweka bayana kilichopo ndani ya ripoti hiyo, habari zisizo rasmi zimekuwa zikidai kuwa tume ya Dk Bashiru imeibua uozo mwingi na hivyo kuweka hisia za wachambuzi wa mambo kuwa kwa utendaji wa mwekitiki wa sasa wa chama hicho huwenda vigogo wengi ndani ya CCM waliotajwa kufuja mali za chama ‘watakula vumbi’.

Siku nne kabla kufanyika mkutano wa leo na kesho wa CCM, mwenyekiti wa chama hicho aliimarisha safu yake ya uongozi kwa kumteua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Nne, Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, jambo linalodaiwa huwenda mkutano wa leo ukatoka na majina hayo katika nyadhifa mpya za uongozi.

Comments

Popular posts from this blog