DAWA ZAVUSHWA KUPITIA MTO WENYE MAMBA MKOANI RUVUMA
Wakazi
wa vijiji vilivyopo kandokando ya mto Ruvuma wilayani Nyasa mkoani
Ruvuma na wafanyakazi wa Bobari ya Dawa (MSD), wakisaidia kushusha
maboksi yenye dawa na kuyaingiza kwenye mtumbwi baada ya kupelekewa na
MSD Kanda ya Iringa leo na baadae kuyapeleka katika Zahanati ya Kijiji
cha Mitomoni.
Maboksi ya dawa yakiingizwa kwenye mtumbwi.
Wakazi wa Kijiji cha Mitomoni wakisubiri mtumbwi ili kuwavusha upande wa pili wa mto Ruvuma.
Dawa zikipelekwa Zahanati ya Mitomoni
Maboksi ya dawa kutoka MSD yakishushwa
Wananchi wakishusha maboksi hayo kutoka katika mtumbwi.
Mkazi wa Kijiji cha Mitomoni Khadija Salum, akizungumzia upatikanaji wa dawa kutoka MSD.
Mkazi wa kijiji hicho, Mbwana Koloma, akizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara na jinsi wanavyopokea dawa kutoka MSD.
Mwenyekiti wa kamati ya Afya wa Kijiji cha Mitomoni Omar Hassan akizungumza wakati wa kupokea dawa hizo.
Mmoja wa viongozi wa Kijiji cha Nakawale, Ima Komba akisaini fomu maalumu ya kupokelea dawa kutoka MSD.
Na Dotto Mwaibale, Ruvuma
WANANCHI
wanaoishi katika Vijiji vya Mkenda na Mitomoni vilivyopo kandokando ya
mto Ruvuma wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wamesema changamoto kubwa
waliyonayo ni
mazingira magumu ya miundo mbinu ambayo inasababisha ugumu wa ufikishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Wakazi
hao wamesema kuwa, mazingira ya kufikisha dawa kwenye vijiji hivyo
hutegemea zaidi usafiri wa kuvuka mto Ruvuma ambapo hulazimika kutumia
boti,ambapo hata hivyo maisha yao yanakuwa na mashaka ndani ya mtumbwi
hiyo ambayo iko wazi kutokana na mto huo kuwa na mamba wengi.
“Changamoto
yetu kubwa ni usafishaji wa dawa kuja hapa kijijini kutokana na
kutegemea zaidi mto huu ambao una mamba wengi, hata mwaka huu mwanzoni
mtumbwi huu mnaouona ulipinduka na watu wakiwapo wauza mitumba waliuawa
na mamba; lakini tunashukuru Bohari ya Dawa (MSD) kwani wao wanaweza
kutuletea dawa kwa wakati” alisema Mwenyekiti wa kamati ya Afya wa
kijiji cha Mitomoni Omar Hassan.
Alisema
ili kuondoa changamoto hiyo, wanaiomba serikali kuhakikisha inaboresha
miundombinu ya barabara, ili dawa hizo zisafirishwe kwa njia ya barabara
badala ya kutegemea mto huo.
Alisema yeye na kamati yake wamekuwa wakipokea dawa mara nne kwa mwaka kutoka MSD na kuzihakiki kwa ajili ya matumizi.
“Pamoja
na changamoto ya miundombinu lakini tumekuwa tukihakikisha dawa
zinazoletwa na MSD zinafika kituoni na kutumika ipasavyo,”alisema.
Alisema
kutoka Songea mjini hadi Kijiji cha Mitomoni, Songea vijijini, katika
kituo hicho cha afya ni km 135 na MSD imekuwa ikihakikisha dawa hizo
zinafika.
Alisema
changamoto zinakuwa kubwa zaidi kipindi cha mvua kwa kuwa miundombinu ya
barabara hadi kufika kivukoni ni tatizo na kuna wakati dawa zinafika
usiku na zinatakiwa kuvushwa usiku huo huo.
Hassan
alisema changamoto hiyo ya mamba katika mto huo anaijua vizuri kwani
mtoto wake Sanifu Omar (27), alipoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati
alipokuwa akisafirisha abiria kwa kutumia mtumbwi.
Mkazi wa
Kijiji cha Mitomoni Khadija Salum alisema wamekuwa wakipata dawa zote
muhimu katika kituoni hicho ikiwemo za mama mjamzito na mtoto bila ya
ubaguzi na kwa wakati.
“Mimi
nina watoto watano kuanzia ujauzito wa kwanza sijawahi kukosa dawa hapa
pamoja na ugumu wa miundombinu lakini dawa zinafika hivyo serikali ione
haja ya kuboresha barabara zetu,” alisema.
Mganga
Mfawidhi wa Zahanati ya Mitomoni, Ivo Hekela, alisema kijiji hicho
kinahudumia agonjwa 12,000 kutoka vijiji vitano ambavyo ni Mitomoni,
Mipotopoto,Konganywita,Mkenda,Uhuru na Mozambique.
Meneja wa
MSD Kanda ya Iringa, John Sipendi, alisema wamekuwa katika changamoto
ya kufikia vituo hivyo vya pembezoni ikiwa ni pamoja na kutumia muda
mrefu kufikisha dawa na wakati wa mvua kukwama kwa magari njiani na
gharama za usafirishaji kuogezeka.
Madereva wa MSD Kanda ya Iringa wamesema wamekuwa wakishindwa kushusha dawa wakati wa mvua za masika kutokana na mto huo kujaa maji hivyo hulazimika kulala kijijini hapo kwa siku mbili hadi tatu.
Comments
Post a Comment