Waziri Mwakyembe atoa ombi hili kwa Wabunge
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amefunguka na kuwataka baadhi ya Wabunge Bungeni kuacha kuwatetea wasanii wanaoimba nyimbo zisizokuwa na maadili kwa kuwa kufanya hivyo kuna pelekea kuonekana taifa la Tanzania kuwa mfu lisilokuwa na utamaduni wake.
Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo (Aprili 10, 2018) kwenye mkutano wa 11 kikao cha sita kinachoendelea kufanyika mkoani Dodoma wakati akijibu swali la Nyongeza kutoka kwa Mbunge Catherine Magige ambaye alitaka kufahamu ni kwanini kamati ya maudhui inashindwa kufanya kazi zake kwa wakati mpaka inafikia muda wasanii wanaachia kazi zao za sanaa ndio wao wanaibuka na kuanza kuwafungia kazi hizo, je wameshindwa kazi ?.
"Kila taifa lina utamaduni wake na lazima liulinde kwa udi na uvumba, tunachokifanya sisi sio kwamba tuna vita na wasanii wetu, hapana. Lakini lengo letu ni kulinda maadili ambayo katika kipindi hiki cha utandawazi kumekuwepo na mmong'onyoko mkubwa katika taifa letu na lazima tuchukue hatua. Tunachokifanya sisi hapa sio jambo jipya duniani, kila mtu anafanya hivyo na hawa wasanii wetu tumeshawasamehe wasirudie tena", amesema Dkt. Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Waziri Mwakyembe ameendelea kwa kusema kwa kutumia baadhi ya nukuu ya Hayati Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere kwamba "Taifa lisilokuwa na utamaduni wake ni taifa mfu'. Sisi hatuwezi kukubali kuwa taifa mfu. Yanayotokea Tanzania yanatokea duniani kote".
Kwa upande mwingine, Waziri Mwakyembe amesema Wizara yake kupitia kamati ya maudhui itaendelea kuzifungia nyimbo zisizokuwa na maadili ili waweze kulinda utamaduni wa taifa la Tanzania.
Comments
Post a Comment