Siwa ya Bunge yakutwa kwenye Flyover
Baada ya watu wenye silaha kuvamia Bunge la Senate la Nigeria na kuiba siwa juzi, hatimaye imekutwa chini ya Barabara ya Juu ‘flyover’ Jijini Abuja baada ya kuonwa na mwananchi aliyekuwa akipita maeneo hayo.
Inadaiwa watu hao waliongozwa na Mbunge Ovie Omo-Agege ambaye amefungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na tuhuma hizo.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Nigeria ameeleza kuwa kitendo hicho ni uhaini na inaashiria kuwa mtuhumiwa, Omo-Agege alikuwa akijaribu kupindua moja ya mihimili ya Serikali ya Nigeria. Siwa ni ishara ya mamlaka ya Bunge hilo na Sheria haziwezi kupitishwa bila kuwepo kwa kifaa hicho.
Licha ya kitendo hicho, Bunge liliendelea na kazi yake kwa kutumia Siwa ya ziada iliyokuwepo bungeni hapo ambapo kabla ya hapo Seneta wa Kaduna, Shehu Sani alivua mkanda wake na kuuweka sehemu ya Siwa hiyo.
Aidha, Chama tawala, APC kimeita tukio hilo kuwa ni shambulio kwa Demokrasia ya nchi hiyo na kutaka waliohusika kukamatwa. Hadi sasa Seneta Omo- Agege anashikiliwa na Polisi akihusishwa moja kwa moja na tukio hilo.
Comments
Post a Comment