Sababu Za Kuwashwa Baada Ya Kuoga
“Wataalamu wa afya ya ngozi pia wanabainisha kuwa kuoga muda mrefu na mara kwa mara, matumizi ya sabuni zenye harufu kali na povu jingi ni mambo mengine yanayochangia kutokea kwa mzio pamoja na ukavu wa ngozi kutokana na uwezo wake wa kuondosha kiasi kikubwa cha mafuta yanayolinda ngozi.
Ili kupunguza hali ya muwasho, “Tumia sabuni zenye mafuta, lakini zisiwe na marashi makali.”
Katika hali ya kawaida kitendo cha kuoga
kinapaswa kuchukuliwa kama jambo la kufurahisha kutokana na ukweli kwamba
huufanya mwili uburudike na kuwa safi. Lakini kwa baadhi ya watu mambo ni
tofauti. Kuoga huwa sawa na karaha.
Moja ya matatizo ya kiafya ambayo
yanayosumbua watu wengi duniani na kuwanyima raha ya maisha, ni tatizo la mwili
kuwasha mara baada ya kuoga. Muwasho baada ya kuoga unaweza kujitokeza mwili
mzima au unaweza kuhusisha baadhi ya sehemu.
Hali hii inaweza kuwa inajitokeza kwa
muda wa dakika chache au inaweza kuchukua muda mrefu na kwa baadhi ya watu,
hili linaweza kuwa tatizo sugu. Ingawa tatizo hili la kiafya ni kama mengine,
lakini baadhi ya watu kwa kukosa taarifa sahihi, hulihusisha na imani potofu.
Ukweli wa mambo ni kwamba kuna sababu
nyingi zinazochochea kutokea kwa tatizo hili na baadhi hazina madhara makubwa
kama vile kuhatarisha kwa maisha.
Pamoja na ukweli wa kisayansi kwamba
asilimia 70 ya mwili wa binadamu ni maji, kwa upande mwingine yanaweza kuwa
chanzo cha matatizo ya kiafya hasa pale yanapokuwa na vitu vinavyosisimua mwili
au kuchochea hali ya kutokea kwa mzio. Siyo jambo la kushangaza kuona kuwa maji
ambayo ni safi na salama kwa kunywa yanaweza kuwa siyo salama kwa kuoga.
SABABU ZA MUWASHO MWILINI
SABABU ZA MUWASHO MWILINI
Miongoni mwa sababu za kutokea kwa
muwasho wa mwili baada ya kuoga ni za kimazingira na sababu zingine zinahusiana
na hitilafu za urithi wa vinasaba vya kijenetiki katika mfumo wa kinga ya mwili
wa mhusika.
Wakati mwingine tatizo hili linaweza
kuwa ni dalili muhimu inayoonyesha baadhi ya magonjwa ya kuambukiza na
yasiyoambukiza kama vile matatizo ya figo, ini, tezi shingo, matatizo ya mfumo
wa damu, kisukari, saratani ya mitoki na msongo wa mawazo.
Baadhi ya tafiti zinabainisha kuwa
sababu nyingine ni pamoja na uchafuzi wa mazingira ya hewa kwa kemikali zenye
sumu zinazopatikana katika moshi wa tumbaku, mifuko ya plastiki, dawa za
kufanyia usafi majumbani, dawa za kuua wadudu, vumbi ya ndani ya nyumba
yanayobeba vimelea vya magonjwa pamoja na uchafuzi wa hewa kwa moshi wa magari
na ule unaozalishwa na viwanda katika maeneo ya mijini.
Vitu hivi huufanya mwili kuathirika na
kutengeneza mazingira ya ndani ambayo yanachochea kutokea kwa muwasho pindi
mwili unapopata msisimuko, hali ambayo hujulikana kama mzio.
Mzio huanza pale mfumo wa kingamwili
unapobainisha kemikali hizi kama mvamizi wa mwili na kuamuru askari wake wajulikanao kama seli
za T-lymphocites na B-lymphocytes kujibu mapigo ya wavamizi kwa kuzalisha
kemikali maalumu zijulikanazo kama immunoglobulin E na prostaglandins ambazo
husababisha kuzalishwa kwa kemikali nyingine kama vile histamine, tryptase
na chymase, kwa lengo la kuvunja nguvu
za kemikali vamizi.
NI KWA NAMNA GANI?
Baadhi ya watafiti wanabainisha kuwa
kutokana na hitilafu za vinasaba vya kijenetiki kunakuwa na ongezeko la kemikali
aina ya Cyclic Adenosine Monophosphate
Phosphodiesterase ambayo inaharibu mfumo wa udhibiti wa seli za kinga
mwili aina ya basophils na seli za mast na kusababisha zisisimuke kupita kiasi na
kuzalisha histamine nyingi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa
mzio.
Watu wengi wana mzio wa vitu mbalimbali
ikiwa ni pamoja na dawa za tiba, kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni,
vipodozi, aina fulani za vyakula, kemikali kadhaa zinazotumika katika
usindikaji wa vyakula, kemikali zinazowekwa katika maji kama vile chlorine
(watergurd), maji ya kuoga yenye chumvi nyingi na kemikali zinazotumika katika
utengenezaji wa nguo, ikiwa ni pamoja na mataulo ya kuogea.
Mapambano kati ya kinga mwili na kile
ambacho mwili hukibainisha kwa makosa kama wavamizi, yanaweza kusababisha
magonjwa ya pumu, muwasho wa ngozi, muwasho wa macho, mafua ya mara kwa mara na
maumivu ya tumbo.
SABABU NYINGINE
Mapambano haya pia yanaweza kusababisha
hali ya mzio dhidi ya vyakula kama vile mayai, maziwa, samaki, nyama, karanga,
vyakula vitokanavyo na unga wa ngano, kahawa, pombe na baadhi ya vyakula na
vinywaji vinavyotengenezwa au kusindikwa viwandani kwa kutumia kemikali. Hali
hii pia inaweza kutokea kutokana na kula vyakula vyenye mchanganyiko wa
vikolezo kama pilau na viungo vingi.
Ulaji wa vyakula vyenye upungufu wa
viinilishe nao unatajwa kuwa unachangia kutokea kwa tatizo la mwili kuwasha
wakati wa kuoga.
Watu wengi hawatumii kiasi cha kutosha
cha matunda, mboga na mafuta salama yanayotokana na mimea au samaki, jambo
ambalo huathiri vibaya afya ya ngozi.Tatizo jingine linalochangia mwili kuwasha wakati wa kuoga ni kutokutumia kiasi cha kutosha cha maji ya kunywa kila siku. Hali hiyo inafanya mwili kuwa na upungufu wa maji na kuathiri vibaya afya ya ngozi na uwezo wake wa kuondosha sumu mwilini.
Ngozi isiyokuwa na afya njema inashindwa
kutunza kiasi cha kutosha cha unyevu na kusababisha ukavu. Ngozi inapokuwa kavu
husisimka kupita kiasi wakati wa kuoga na kusababisha muwasho. Sababu ya
mwili kuwasha baada ya kuoga ni kuishi katika hali ya msongo wa mawazo
inayosababishwa na hofu, wasiwasi na sonona.
Tatizo jingine linalosisimua mwili na
kusababisha muwasho wakati wa kuoga ni kujisugua kupita kiasi au kujisugua
wakati wa kujifuta kwa taulo baada ya kuoga.
Kwa kawaida seli za ngozi zilizokufa, jasho na vumbi ndivyo
vinasababisha mwili kuchafuka.
Lakini uchafu huo huondoka mwilini
tunapooga na nguvu nyingi hazihitajiki ili kuondosha uchafu na taka mwili juu
ya ngozi. Matumizi ya nguvu nyingi na kusugua ngozi sana, husababisha madhara
kwenye ngozi na kusababisha muwasho au ukavu wa ngozi kwa kuondosha mafuta
yanayolinda usalama wa ngozi.
Watu wenye tatizo hili wanaweza kufanya
mazoezi mepesi kabla ya kuoga ili kupasha mwili joto au kupaka lotion ili
kuifanya ngozi kuwa na unyevu na kupunguza hali ya ukavu wa ngozi.
source:manyanda
Comments
Post a Comment