REKODI 3 NDOA YA KIBA!

DAR ES SALAAM: Wakati mkali wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ amefunga ndoa leo pande za Mombasa nchini Kenya, nyumbani kwa bibi harusi, Amina Khaleef, imeelezwa kuwa ndoa hiyo inatarajia kuandika rekodi ya mambo makubwa matatu.

Akizungumza na Gazeti la Amani, mmoja wa mameneja wa mwanamuziki huyo, Aidan Sefu, alisema tayari wamelipwa mamilioni ya fedha na moja ya luninga ya hapa Tanzania kurekodi na kurusha live harusi hiyo.“Itakuwa kitu kikubwa sana, ni harusi ya aina yake hivyo nisingependa kuongea sana lakini watu wataona,” alisema Aidan.

Kama hiyo haitoshi, Amani lilielezwa kuwa miongoni mwa rekodi zinazotarajiwa kuandikwa katika harusi hiyo ni pamoja na kukodiwa ndege maalumu ya kwenda Mombasa na kurudi Bongo. “Kutakuwa na utofauti mkubwa kwani Ali anatarajiwa kukodi ndege kumpeleka kama bwana harusi na ndege ya kumrudisha akiwa tayari na kifaa chake ili kuja kumalizia sherehe huku mwisho wa mwezi,” alisema mnyetishaji wetu.

Pia mnyetishaji huyo alisema rekodi nyingine inayotarajiwa kuwekwa katika harusi hiyo ni pamoja na kuhudhuriwa na viongozi wengi wa serikali jijini Mombasa na baadaye Tanzania. Kwa upande wa Tanzania, anatarajiwa kuhudhuria Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Salma. Imeelezwa pia, kutakuwa na supraizi bab’kubwa ya wasanii mbalimbali wengi wa Kimataifa katika harusi hiyo.

Comments

Popular posts from this blog