Mamba akutwa katika bwawa la kuogelea Florida, Marekani


Polisi katika jimbo la Florida, Marekani wamesema mamba wa urefu wa futi 11 alipatikana kwenye bwawa la kuogelea la familia moja katika jumba hilo.

Polisi wamepakia picha za mamba huyo mtandaoni, Wakazi wa Nokomis waliwapigia simu polisi na kuomba usaidizi baada ya kumgundua mnyama huyo.

Afisa wa polisi wa eneo la Sarasota alipakia mtandaoni picha ya afisa wa wanyama aliyeitwa kumnasa akiwa anamburuta mnyama huyo kutoka kwenye maji Jumamosi.

Polisi wanasema mamba huyo alifanikiwa kupita kwenye uzio uliokuwepo na kuingia kwenye bwawa hilo, Mamba nchini Marekani kwa kawaida hukua hadi kuwa na futi kati ya 11 na 15 na wanaweza kuwa na uzani wa kilo 454.


Mamba wa Marekani hupatikana mashariki mwa Marekani katika majimbo ya Florida na Louisiana, kila jimbo likiwa na zaidi ya mamba milioni moja.

Eneo la kusini mwa Florida ndilo pekee ambalo mamba wa Marekani na mamba wa kawaida huishi kwa pamoja.

Ingawa awali walikuwa wameorodheshwa kama wanyama walio hatarini chini ya sheria za mwaka 1973, idadi yao iliongezeka sana kwa haraka na kufikia mwaka 1987 wakaondolewa kutoka kwenye orodha hiyo.

Inakadiriwa kwamba kuna mamba milioni moja hivi Florida, na wengine milioni moja Louisiana.

Comments

Popular posts from this blog