Lowassa asema hatapoteza muda kwenda kupimwa DNA
- Get link
- X
- Other Apps
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema hamtambui mwanamke aliyejitambulisha juzi kama binti yake aliyetelekezwa na kwamba hatapoteza muda kwenda kupimwa vinasaba (DNA), kama msichana huyo alivyotaka.
Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu, Lowassa ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuwa kinachofanyika kwenye zoezi hilo ni siasa.
Msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma alijitokeza hadharani juzi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kutelekezwa na Lowassa ambaye alisema ni baba yake, kwa kuambiwa na mama yake mzazi.
"Wewe unamwamini kweli huyo msichana? Angekuwa mwanangu kweli ningeshamchukua muda mrefu, kwanza wala simjui naona siasa zinaingizwa hapo," alisema.
Alipoulizwa kama yuko tayari kupimwa DNA ili ukweli ujulikane, Lowassa alijibu "Kupima DNA huo ni upuuzi. Yaani nipoteze muda wangu kwenda kufanya upuuzi huo? Siko tayari."
Msichana huyo ni miongoni mwa mamia ya wanawake waliojitokeza kuanzia Jumatatu kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.
Makonda alitaka wanawake waliotelekezewa watoto na waume zao wafike ofisini kwake kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, kwa ajili ya kuzungumza na wanasheria, maofisa wa ustawi wa jamii na askari polisi wa Dawati la Jinsia. Siku hizo zitaisha kesho baada ya kuongezwa.
Akizungumza na vyombo vya habari juzi, Fatuma alisema yuko tayari kupima vinasaba na Lowassa ili kuthibitisha kama kweli ni baba yake na kwamba alimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.
"Nilipeleka barua Ikulu kuomba kuonana na baba (Lowassa) kipindi akiwa Waziri Mkuu (2006-2008) lakini niliitwa mimi na mama katika klabu ya Mamba iliyopo Kinondoni," alisema Fatuma.
"(Hapo) alikuja mwanaume akiwa kwenye gari lenye vioo vyeusi akatuhoji mimi na mama, akaondoka hakutupa majibu yoyote hadi leo."
Kuhusu madai hayo, Lowassa alisisitiza kuwa kama kweli angekuwa mtoto wake asingesita kumchukua.
"Wala simjui, anasema ameshindwa kuniona wakati ana miaka 31, wewe unaamini kweli ameshindwa kuniona? Mbona wewe umenitafuta na umenipata na unaongea na mimi kwenye simu," alisema Lowassa.
"Hizo ni siasa zinazolenga kuchafuana."
Pia katika maelezo yake, Fatuma alidai kuwa aliwahi kukutana na mtoto wa Lowassa aitwaye Fred na alimwahidi kumsaidia lakini hadi sasa amekuwa kimya.
FURIKA VIWANJA
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, mamia ya wanawake walifurika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuanzia saa 11 alfajiri ili kupata namba.
Kutokana na mwitikio kuwa mkubwa, wanawake waliofika kuanzia saa 1:00 asubuhi walikuwa hawajapata namba hadi saa 8:00 mchana, huku waliojiandikisha wakiwa zaidi ya 500.
Hata mvua iliyoanza kunyesha majira ya saa 6:00 mchana ikiambatana na radi haikuwazuia wanawake wakiwa na watoto wao wadogo wa chini ya miaka mitatu kuendelea kupanga foleni kusubiri huduma.
Baadhi ya wanawake hao walilazimika kuingia gharama za kununua miavuli ili kujisitiri na mvua hiyo ili kutimiza kusudi lillilowapeleka eneo hilo.
Kutokana na mwitikio mkubwa wa wanawake hao, Makonda alilazimika kuongeza siku za kuwahudumia kutoka tatu zilizokuwa zimepangwa hadi kufikia tano.
Makonda alisema wanawake hao watapatiwa msaada wa kisheria kila mmoja ndani ya siku hizo tano na kwamba wanaume watakaotajwa kuhusika kuwatelekeza wataitwa kuhojiwa. Walishaanza kuitwa.
Alisema wanaume watakaotajwa watatakiwa kufika katika ofisi hizo kueleza sababu za kutelekeza watoto na endapo kutakuwepo na utata kuhusu uhalali wa mtoto vipimo vya Vinasaba vya Binadamu (DNA) vitatumika.
Kadhalika, aliahidi kuwatangaza wanaume watakaokaidi kuwatunza watoto wao ili jamii iwatambue.
"Tutangaza majina ya wanawaume wote wataotajwa kuhusika na hawa watoto ili jamii iwatambue," alisema Pia aliwatia moyo wanawake hao kwa kusema tendo la kuzaa si tendo la laana bali ni tendo la baraka na kila mmoja anatakiwa kuliheshimu.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment