TFDA kuzuia soseji kutoka Afrika Kusini zenye bakteria

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imesema itazuia uingizaji wa soseji kutoka Afrika Kusini zilizobainika kuwa na bakteria aina ya listeria.

Uamuzi wa TFDA unatokana na soseji hizo aina ya Polony kubainika kuwa na aina hiyo ya bakteria wanaosababisha ugonjwa wa listeriosis uliosababisha vifo vya watu 180 nchini Afrika Kusini.

Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza akizungumza na Mwananchi jana alisema mamlaka hiyo inalifanyia kazi suala hilo ikiwa ni pamoja na kuzuia uingizwaji wa soseji hizo nchini, “Tunalifanyia kazi kwa kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama soseji husika zipo katika soko,” alisema.

Soseji hizo kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na vyombo kadhaa vya kimataifa zinatengenezwa na kiwanda cha tiger brands unit enterprises na cha RCL foods vyote vya Afrika Kusini.

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Aaron Motsoaledi alikaririwa na mitandao ya kijamii akisema ameagiza kuondolewa sokoni soseji hizo, huku akiwashauri wananchi kuacha kula.

Motsoaledi alisema ingawa kiwanda cha RCL hakijatajwa kama chanzo cha ugonjwa huo, kitengo chake kinafanyiwa uchunguzi, Ugonjwa wa listeriosis uliibuka Desemba mwaka jana na umeshasababisha vifo vya watu 180.

Akiuchambua ugonjwa huo, daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, George Kanani alisema listeria ni aina ya bakteria ambao hupatikana kwenye maji, udongo na kinyesi. Alisema binadamu huambukizwa wanapotumia vyakula au maji yenye bakteria hao, “Sababu kuu zinazosababisha listeriasis ni nyama na maziwa mabichi,” alisema.

Dk Kanani alisema bakteria hao ni hatari na husababisha kifo wanaposhambulia mfumo wa fahamu na damu.

Alisema wanaoathiriwa kwa urahisi na bakteria hao ni watu wenye kinga ya mwili hafifu, wenye umri wa miaka zaidi ya 65, wajawazito, wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), wenye matatizo ya figo, kisukari na waliofanyiwa upasuaji.

Akielezea namna bakteria walivyoingia katika soseji, Dk Kanani alisema yawezekana kulikuwa na shida katika usafi kiwandani wakati wa kuziandaa.

“Njia ya kuepuka ni usafi, kusafisha chakula, kuacha kutumia mboga za majani mbichi, kula vyakula vilivyopikwa vizuri. Bidhaa za nyama zinatakiwa kuandaliwa katika mazingira salama,” alisema.

Tamra Capstick-Dale, mhudumu katika duka kubwa (supamaketi) nchini Afrika Kusini la Pick n Pay alikaririwa katika mitandao ya vyombo vya habari vya kimataifa akisema wameshaziondoa soseji hizo katika maduka yao.

Tovuti ya kampuni ya Tiger Brands imeweka orodha ya nchi ambazo bidhaa zake husambazwa, miongoni mwa hizo ni Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog