Tanzia:Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma mjini afariki dunia Muhimbili

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Dkt. Amani Walid Kabourou amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dkt. Kabourou ambaye alizaliwa Mei 23, 1949, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini (CHADEMA) kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Aidha, Dkt. Kabourou amewahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki akiiwakilisha Tanzania kuanzia Juni 05, 2007 hadi Juni 04, 2012.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa sasa wa Kigoma Mjini amesema kwao huo ni msiba mkubwa, na umewaacha na majonzi tele.

“Tumeamka asubuhi na habari za kusikitisha kuwa Dkt. Amani Walid Kabourou, Mbunge Mstaafu wa Kigoma Mjini ametangulia mbele ya haki. Hakika ni msiba mkubwa kwetu. Mola ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” ameandika Zitto.

Comments

Popular posts from this blog